Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais- TAMISEMI Zainab Katimba ameshuhudia utiaji Saini Mkataba wa Ujenzi wa Soko la Mwanga pamoja na Soko la Samaki Katonga yote yakiwa katika Manispaa ya Kigoma Ujiji ikiwa ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji ya Tanzania (TACTIC).
Akimwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Naibu Waziri Katimba amesema lengo la miradi ya TACTIC ni kuziwezesha Halmashauri za Miji nchini kutoa huduma bora kwa Wananchi.
Amesema ni matarajio ya serikali kuwa miradi hiyo iliyosainiwa utekelezaji wake italeta mabadiliko chanya kwa wananchi kwa kuwawekea mazingira bora ya kibiashara, kurahisisha kupata huduma za kimasoko pamoja na kuchangia ongezeko la mapato kwa Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Miradi hiyo, Mwakilishi wa Mkurugenzi amkuu TARURA Mha. Hampher Kanyenye amesema Mkataba wa ujenzi wa masoko hayo mawili unathamani ya Shilingi Bil. 16.4 na utekelezaji wake utafanyika katika kipindi cha miezi 12 kuanzia Novemba 15, 2024 ujenzi ukifanywa na wakandarasi wazawa M/S Asabhi Co. Ltd. na Pioneer Builders Ltd.
Amesema kutokana na ujenzi wa Soko la Mwanga, jumla ya wafanyabiashara 4140 watanufaika kupitia shughuli za kibiashara ambapo awali soko lilijumuisha wafanyabiashara 1246, ujenzi wa vizimba 1000, maduka 3040, migahawa ya mama lishe 100, kituo cha polisi huku mapato yakikadiriwa kufikia bil. 1.4.
Ameitaja miundombinu mingine itakayojengwa katika soko hilo kuwa ni Ofisi, ukumbi wa Mikutano, maegesho ya magari na pikipiki, vyoo vya kulipia na maeneo ya kupumzikia.
Amesema ujenzi wa Soko la Samaki Katonga utatoa fursa kwa wafanyabiashara 2000 kunufaika kutoka 270 wa awali huku matarajio ikiwa kujenga vizimba 300, maduka 800, vyumba 10 vya kutunzia samaki pamoja na ujenzi wa eneo la kukaushia samaki lenye urefu wa mita 5256 pamoja na eneo la kuhifadhia mitumbwi, vyoo pamoja na Ofisi za soko.
Aidha Mha. Kanyenye amesema soko hilo litakapokamilika matarajio ni kuongezeka kwa makusanyo kutoka Shilingi Mil. 31.5 na hadi kufikia Mil.183.2, jambo litakaloemdelea kuimarisha mapato katika Manispaa ya Kigoma Ujiji na Taifa kwa ujumla.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa