UJENZI WA KITUO KIDOGO CHA KUPOZA UMEME KILICHOPO KIDAHWE JIRANI NA MJI WA KIGOMA
Ujenzi wa njia ya kusafirisha Msongo wa Umeme wa Kilovoti 400 kutoka Nyakanazi hadi Kidahwe wenye Thamani ya Shilingi Bilioni 434.9 umefikia zaidi ya 80% ambapo kukamilika kwa Mradi huo kunatajwa kuwa suluhisho la kudumu kutokana na mkoa kuwa na changamoto ya muda mrefu ya utoshelevu wa upatikanaji huduma ya Umeme.
Mradi huo unahusisha miradi mitatu ambapo kwa upande wa mradi wa ujenzi wa njia ya Umeme Nyakanazi hadi Kidahwe ulioanza kutekeleza Januari 2022 na Mkandarasi M/s TATA Projects Ltd kutoka nchini India, umefikia 84% na unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 30, 2024.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu amedhamiria kuwaondolea wananchi wa mkoa wa Kigoma adha ya ukosefu wa umeme kwa kuidhinisha ujenzi wa mfumo huo utakaoingiza umeme wa kutosha na wenye uhakika katika kuendesha shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaipunguzia hasara Serikali kwa kuachana na matumizi ya mafuta yanayofikia kiasi cha lita 30,000 kwa siku kwa ajili ya uendeshaji wa jenereta zinazozalisha Umeme unaotumika mkoani Kigoma,
‘’Matumizi ya jenereta yametupeleka kwenye mgao wa umeme kutokana na kutotosheleza kwa nishati hiyo, jambo lililochangia kwa kiasi kikubwa mkoa kukosa wawekezaji upande wa Sekta ya viwanda jambo linaloikosesha nchi kiasi kikubwa cha mapato’’ amesema.
Amefafanua kuwa, mpaka sasa mkoa umepokea maombi ya wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kupitia sekta za viwanda ambao wanadhamira ya kuwekeza kutokana na kujihakikishia uwepo kwa umeme wa kutosha na wenye uhakika jambo litakalotoa fursa kwa wakazi kujipatia ajira za muda na zile za kudumu.
‘‘Ifahamike kuwa serikali inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Tabora hadi Kigoma yenye urefu wa Km. 506, ujenzi wa kiwanda cha kutengenezea Meli pamoja viwanda vingine vilivyopo vya kuchakata bidhaa mbalimbali ambavyo vyote hivyo vitahitaji kuendeshwa kwa kutumia umeme wa uhakika’’ ameendelea kufafanua Andengenye.
Mhandisi wa ujenzi wa miundombinu ya Usafirishaji wa Msongo wa Umeme Nyakanazi hadi Kidahwe Nyango Magesa amesema kazi za usanifu wa mradi huo zimefikia 99% Manunuzi ya vifaa 99% pamoja na Ujenzi kufikia 84.4%.
mhandisi Magesa ameitaja miradi jumuish inayotekelezwa pamoja na mradi wa kusafirisha umeme Nyakanazi hadi Kidahwe kuwa ni pamoja na mradi ni ujenzi wa kituo cha kupoza umeme KV 400/132/33 kilichopo mkoani Kigoma eneo la Kidahwe pamoja na upanuzi wa kituo cha kupoza Umeme Nyakanazi unaotekelezwa kwa thamani ya Shilingi Bil.164 na Mkandarasi M/s Sean and Hyuson kutoka Korea.
Ameutaja mradi mwingine unaotekelezwa sambamba na mradi huo ni ujenzi wa njia za usambazaji Msongo wa Umeme wa KV 33 na Voti 400 kwa Thamani ya Shilingi Bil. 11.5 ukitekelezwa na Mkandarasi M/s Giza Cable Industries kutoka nchini Misri pamoja na ujenzi wa Kituo cha kupoza Umeme Kigoma na Kasulu unaotekelezwa kwa Gharama ya Takribani Shilingi Bil. 9.2 ambapo hatua iliyofikiwa ni usanifu wa michoro, uchunguzi wa udongo kwa ajili ya kuona iwapo maeneo husika yanafaa kwa ajili ya ujenzi wa miradi hiyo.
Mha. Magesa amesema ujenzi wa njia za usambazaji wa Umeme wa msongo wa kilovoti 33 na voti 400 utakapokamilika utavinufaisha vijiji vya Matendo, Kidahwe, Ngaraganza na Matyazo wilaya ya Kigoma vijijini.
Vijiji vitakavyonufaika kwa wilaya ya Kasulu ni Makere, Nyachenda, Titye, Kitagata, Nyamidaho, Mvugwe, Nyarugusu, Muzye, Bugaga na Kasangezi ambapo kwa Halamshauri ya Mji ni Kanazi, Nyantare, Nyumbigwa na Bugaga.
Mhandisi Magesa amesema zoezi la ulipaji wa fidia kwa maeneo yaliyopitiwa na Mradi huo limekamilika kwa Asilimia 91 ambapo kiasi cha Shilingi Bil. 2.32 kimelipwa kwa wananchi ambao maeneo yao yamepitiwa na mradi na kwa wanaoendelea kuthibitisha taarifa zao watapokea malipo kabla ya mwishoni mwa Mwezi Agosti 2024.
Stephano Gwarema Mkazi wa Kijiji cha Rusesa amesema ameridhishwa na kasi ya serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususani suala la kuimarisha huduma za Umeme, Afya, Maji na barabara katika maeneo ya vijijini.
Kazi zinazoendelea kufanywa na serikali tumeridhishwa nazo na nitoe wito kwa wananchi wenzangu tuendelee kutunza miundombinu hii ili iweze kudumu kwa ajili ya matumizi ya sasa na vizazi vihavyo.
‘‘Mfumo huu wa Umeme unaotekelezwa mkoani Kigoma utakapokamilika utasaidia uwepo wa viwanda vitakavyoweza kutupatia ajira wakazi wa Kigoma na kujiimarisha kiuchumi ili tuweze kumudu kuendesha maisha’’ amesema Gwarema.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa