Shule ya Sekondari ya Wasichana Kakonko ikiwa ni ya mchepuo wa Sayansi, ilianzishwa mwaka 2022 ikiwa na Wanafunzi 64, kutoka kwenye Kata zote 13 za wilaya hiyo hususani wenye ufaulu wa wastani wa A na B kwa matokeo ya Darasa la Saba, imetajwa kuwa suluhisho kwa upatikanaji wa Elimu Bora kwa watoto wa kike wilayani humo.
Shule hii ya kwanza kutoa huduma ya Bweni kwa wanafunzi wa kike, ilianzishwa kwa kutumia majengo yaliyoachwa na Mkandarasi wa Ujenzi wa Barabara kutoka Nyakanazi hadi Kabingo, ambapo majengo hayo yanatumika kwa ajili ya jengo la utawala na nyumba za walimu.
Mpaka sasa Kakonko wasichana Sekondari ina madarasa 12, ikiwa na wanafunzi 268 ambapo kwa mtihani wa kidato cha Pili 2023, jumla ya wanafunzi 28 walipata wastani wa daraja la kwanza, daraja la Pili 18 na daraja la tatu wakiwa 11 huku daraja la nne wakiwa 9.
Upakee wa Shule hiyo ni uwepo wa miundombinu bora ya kisasa sambamba na uhakika wa upatikanaji wa Maji, Umeme na mazingira rafiki na endelevu kitaaluma kwa watoto wa kike, ambapo ujenzi wake mpaka sasa umegharimu kiasi cha Shilingi 620,934,323 fedha kutoka Serikali Kuu.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Dkt. Godfrey Kayombo alisema Serikali ya Awamu ya Sita kwa kipindi cha Miaka mitatu (3) imeelekeza zaidi ya Shilingi Bil. 39.8 kwa lengo la kutekeleza miradi ambapo katika Fedha hizo kiasi cha Shilingi Bil.18 kinatekeleza miradi ya Elimu.
Alisema kutokana na Fedha hizo wamefanikiwa kukamilisha Ujenzi wa Shule mbili za Msingi na nyingine mbili za sekondari huku fedha nyingine zikielekezwa kwenye ujenzi wa matundu ya vyoo na ukarabati wa madarasa katika shule mbalimbali ikiwemo shule ya Kakonko wasichana Sekondari.
Akizitaja changamoto zilizopo shuleni hapo, Mwalimu Anatolia alisema mpaka sasa kunauhitaji wa bweni moja, maabara sambamba na ukamilishwaji wa bwalo la kulia chakula kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo.
‘‘Kulingana na ubora wa shule, hali ya malezi pamoja na kasi ya utoaji wa Taaluma, kila mzazi anatamani mtoto wake achaguliwe kusoma katika shule hii, hivyo tunaendelea kutoa wito kwa wakazi kuweka mazingira rafiki kwa watoto wao kushiriki vipindi darasani kwa ngazi ya elimu msingi ili waweze kupata wastani utakaowaruhusu kusoma katika shule hii’’
Aidha Mwalimu Anatolia alisema mpaka sasa shughuli za ujenzi wa shule hiyo zinazoendelea ni pamoja na ujenzi wa Bweni litakalochukua wanafunzi 120 ukiwa na Thamani ya Shilingi 142, 934,333 zinazotolewa kwa awamu kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania aambapo mpaka sasa zimepokelewa shilingi 132,906,000 ambapo ujenzi huo umekamilika kwa zaidi ya Asilimia Tisini huku bweni hilo likiwa linatumika.
Aliutaja ujenzi mwingine unaoendelea shuleni hapo ni ujenzi wa Bwalo wenye Thamani ya Shilingi 150,000,000 ambapo ujenzi huo unaendelea kutokana kupatika kwa fedha za awali kiasi cha Shilingi 40,000,000 kutoka Serikali kuu na 40,000,000 kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo.
Alfredy Elias Diwani wa Kata ya Kanyonza inakopatikana shule hiyo alisema kabla ya uwepo wa shule hiyo, huduma ya upatikanaji wa Elimu kwa wanafunzi wa kike wenye ufaulu mkubwa ilikuwa inalazimu wachaguliwe kwenda katika shule iliyopo katika wilaya ya Kibondo au Mkoani Tabora.
Alisema wazazi wenye watoto wanaosoma katika shule hiyo wameondokana na adha ya watoto wao kuishi kwenye nyumba za kupanga, gharama za nauli za kuwapeleka na kuwarudisha shuleni, sambamba na huduma za kununua vyakula mara kwa mara.
Thobias Gabriel ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Kanyonza alisema sambamba na kuimarika kwa mazingira bora na salama ya kitaaluma kwa wanafunzi hao, uwepo wa shule hiyo umetoa fursa kwa wakazi wa jirani kupata ajira za muda kwenye ujenzi wa shule sambamba na kuuza bidhaa zao kwa walimu na wanafunzi wa shule hiyo.
Sharafat Ahmad Mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza katika shule hiyo alisema uwepo wa Shule hiyo unawapa fursa ya kutumia muda mwingi kujisomea kwa saabu ya kuishi mazingira ya shuleni tofauti na wenzao wanaosoma shule za kutwa kwani hujikuta wakilazimika kutumia muda wa ziada kufanya kazi za nyumbani badala ya kujisomea.
‘’Hapa hatukabiliani na changamoto ya muda na namna ya kufika shuleni hali kadhalika tunatumia muda wa usiku kujisomea jambo ambalo ni tofauti kwa wale wanaokaa majumbani kutokana na changamoto ya uhakika wa uwepo wa Umeme au mazingira tulivu’’ alisema Sharafat.
Naye Mariam Amos mwanafunzi wa kidato cha Tatu alisema kusoma katika shule hiyo, kunawaepusha na vishawishi ambavyo wangevipata iwapo wangesoma shule za kutwa hususani katika mazingira ya nyumba za kupanga sambamba na maeneo ya mitaani ambapo baadhi ya watu wasio waaadilifu huwafuata na kuwarubuni watoto wa kike kwa nia ya kufanya vitendo vya ngono.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa