UFAFANUZI KUHUSU SAMAKI WANAOHARIBIKA (MIGEBUKA) NA WANAODHANIWA KUWA WAMEVULIWA KWA SUMU
Posted on: May 20th, 2017
Kumekuwa na uvumi kuwa wavuvi Mkoani Kigoma hutumia sumu kuvua samaki ndani ya Ziwa Tanga hivyo samaki wengi wanaouzwa wanadhaniwa kuwa na sumu jambo ambalo ni hatari kwa Afya ya binadamu lakini pia kwa mazao ya ziwani kama samaki na dagaa.
Tunapenda kuwatoa hofu wananchi kuwa hakuna samaki wanaovuliwa kwa sumu na wala hakuna Uvuvi wa kutumia sumu unaofanyika katika Ziwa Tanganyika Mkoani Kigoma. Jambo la Msingi wananchi wanashauriwa kuwachunguza samaki kabla ya kuwanunua ili kujiridisha ubora wa samaki hao kwani wengi wao huharibika kutokana na sababu nyingi.
Zana zinazotumika kuvulia samaki katika Ziwa Tanganyika Mkoani Kigoma ni zile zinazokubalika kwa Mujibu wa Sheria ya Uvuvi namba 22 ya Mwaka 2003, Ibara ya 17(f.) na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009, Kanuni namba 66(1)(a)-(x), (2)-(4). Zana hizo ni pamoja na Liftnet (KIPE), Ringnet, Kachinga/Longline/Hand and Line na Makila.
Aidha pia ikumbukwe kuwa wavuvi wa zana zote hizi wanapaswa kuzingatia Sheria na kanuni zilizozowekwa ili kuhifadhi rasilimali ya uvuvi iwe endelevu. Zana zote tajwa hapo juu zikikamata samaki hupandishwa mtumbwini saa hiyo hiyo isipokuwa zana ya Makila ambayo huachwa hadi asubuhi ndipo huteguliwa/hupandishwa kwenye chombo (maramoja kwa usiku mzima).
Hivyo, samaki wote walio kamatwa mapema/masaa ya mwanzo hufa kutokana na kukabwa kwenye mapezi “Gills” na wavu (mesh hole) hivyo huanza kuharibika na kwa vile wako ndani ya maji, kasi yake ya kuharibika huwa kubwa zaidi (high decaying speed) kuliko zana zinazokamata na kuteguliwa/kupandisha samaki kwenye chombo muda huo huo.
Kitaalam, samaki akiwa amekufa anaoza haraka sana ndani ya maji kuliko akiwekwa sehemu kavu. Hivyo, samaki hao wanafikishwa mialoni wakiwa tayari wameanza kuharibika kwa kiasi kikubwa, na kutokana na kutokuwa na barafu na vyombo vya kisasa vya kuhifadhia, wachuuzi nao wanazunguka nao kwa muda mrefu kutafuta wateja Sokoni, mitaani na katika majumba ya watu hata hivyo uhifadhi wake si mzuri kwani hawana nyenzo bora za kuwahifadhi na matokeo yake wanamfikia mlaji wa mwisho wakiwa wameharibika sana.
Aidha, kwa mujibu wa Sheria namba 22 ya Uvuvi ya Mwaka 2003, na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009, Kanuni namba 47(3) (a.) inaelekeza namna ya kumkagua samaki aliyevuliwa kwa sumu, kuna vitu vinavyohakikiwa ili kujua kama amevuliwa kwa sumu au laa. Timu ya wataalam ya Mkoa imekuwa ikikagua samaki wote wanao/waliohisiwa kuvuliwa kwa sumu, hakuna hata mmoja mwenye sifa ya kuvuliwa kwa sumu isipokuwa wameoza kwa kukaa mda mrefu bila nyenzo za kumuhifadhi.
Hatua zinazochukuliwa kukabiliana na Tatizo
Kumekuwa na utoaji wa elimu endelevu kwa wadau kupitia vikao na wavuvi wa Makila na wavuvi wa zana nyinginezo ambapo wameelekezwa mambo mbalimbali ili kuepuka uaribifu wa samaki.
Kwaza, iwapo wavuvi wataendelea kutega kuanzia saa kumi na moja jioni wameshauriwa kupandisha/kutegua mitego yao kila baada ya masaa matatu ili kuwatoa samaki waliokamatwa kwenye mtego na kuwaweka kwenye vyombo ndani ya mtumbwi kisha kutega zana tena. Hii inaweza kusaidia kupunguza kiwango cha kuharibika kwa samaki kwa kuwa hali ya nje ya maji ni ya upepo na baridi zaidi ukilinganisha na joto la ndani ya maji wakati wa usiku.
Pili, wavuvi wameelekezwa kuwa zana za makila zichelewe kwenda kutegwa ziwai, kwa maana ya mitumbwi kupandisha ziwani kuanzia muda wa saa tatu usiku ili zana itegwe saa tano usiku na kuwa na mda mfupi ndani ya maji ikikamata samaki.
Tatu, Samaki wote watakaoletwa mwaloni wakiwa wameoza, hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa mujibu wa Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009, Kanuni namba 72(c.), (f.) na (i.). Ukaguzi wa mazao ya samaki utaendelea kwenye mialo (organoleptic assessment of landed fish) kwa kutimiza matakwa ya kifungu 84(8) cha Kanuni ya uvuvi ya mwaka 2009.
Aidha, Serikali ya Mkoa wa Kigoma inafanya mikakati ya kudumu katika kukabiliana na upotevu wa mazao ya uvuvi ziwa Tanganyika (Post-harvest losses); mikakati hiyo ni pamoja na kukamilisha mitambo ya kuzalisha barafu (Ice blocks and Ice Flakes) katika mwalo wa Kibirizi, kusimamia Sheria namba 22 ya Uvuvi ya Mwaka 2003 na Kanuni zake za Mwaka 2009 katika kupambana na zana haramu na mazao yasiyo na kiwango kinachokubalika. Wavuvi na wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi kuboresha vifaa vya kuhifadhia samaki wakati wa uvuvi mfano kuwa na Cold Boxes ili kuhifadhi samaki wote waliovuliwa kabla ya kuletwa mwaloni na maboksi ya barafu wanapopelekwa sokoni.
Upotevu wa ubora wa mazao ya uvuvi (Post-harvest losses) upo kwa aina zote za uvuvi ndani ya ziwa Tanganyika, kinachotofautiana ni kiwango cha upotevu (Asilimia za kuharibika kwa samaki/dagaa). Jambo hili linaweza kupunguzwa kwa kiasi kikubwa ikiwa nyenzo bora za uhifadhi zitapatikana kwa urahisi na bei nafuu kwa wadau wa uvuvi. Hata hivyo, Sheria namba 22 ya Uvuvi na Kanuni zake za Uvuvi za mwaka 2009 zitaendelea kusimamiwa ipasavyo na ni jukumu la kila mvuvi halali kufanya kila tahadhari ili kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi.