Mkoa wa kigoma ni miongoni mwa Mikoa iliyoainishwa na Wizara ya Afya kuwa na kiwango kikubwa cha Maambukizi ya Malaria nchini na kuingizwa kwenye Mpango Mkakati wa Malaria wa Mwaka 2021/2025.
Kupitia hotuba ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (Mb), kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2022/2023, Serikali imeanzisha na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na maambukizi ya Malaria ikiwemo uanzishwaji wa vituo Maalum vya kufuatilia wingi (Destiny), aina (Species), na uwepo wa vimelea vya Malaria (Sporozoites) kwenye miili ya Mbu waenezao Malaria.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye kwa kushirikiana na watendaji walio chini ya Wizara ya Afya, wameendelea kusimamia na kutekeleza mipango mbalimbali ya kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa Malaria katika Wilaya za Kasulu, Kibondo, Manispaa ya Kigoma Ujiji, Uvinza na Kakonko ikiwa ni maeneo yaliyobainishwa kuwa na ongezeko kubwa la maambukizi nchini.
Kwa pamoja wameendelea kusimamia mazoezi ya ugawaji wa vyandarua, usambazaji wa Dawa Mseto (ALu) za kutibu malaria, vipimo vya haraka vya malaria (mRDT), dawa za kutibu malaria kali, ufuatiliaji na udhibiti wa maralia kwa akina Mama wajawazito pamoja na upuliziaji wa dawa ya ukoko majumbani katika wilaya za Kasulu na Kibondo.
Mojawapo ya kazi nzuri iliyofanywa na Viongozi wetu na wataalamu wa Afya mkoani hapa ni kusimamia na kufanikisha Zoezi la unyunyiziaji wa kiuatilifu ukoko majumbani. Zoezi hilo limefanyika kwa mafanikio makubwa na kupunguza kiwango cha maambuziki ya malari ambapo mwaka 2018 hadi 2021 maambukizi yameendelea kushuka kutoka Asilimia 33.1 hadi 12.5 kwa wilaya ya Kasulu na Asilimia 24.1 hadi 12.5 kwa wilaya ya Kibondo.
Mazoezi mengine ya kupambana na maambukizi ya Malaria yanaendelea kufanyika na kusimamiwa kwa ukaribu kama ugawaji wa vyandarua, kushusha kiwango cha maambukizi ya Malaria kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, kufanya tafifti mbalimbali zenye lengo la kudhibiti mbu waenezao maralia nk.
Wakati Serikali inaendelea kutoa huduma hizo, huku watendaji wake mkoani Kigoma wakiendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Mipango na kazi mbalimbali za udhibiti wa Maralia, ni jukumu la Wananchi kuheshimu kuthamini na kuzingatia hatua zinazochukuliwa kisha kuunga mkono mikakati hiyo kwa usalama wa afya na ustawi wa Jamii kwa ujumla.
Baadhi ya wakazi ama kwa kutokujua au kwa kufanya makususdi, wamekuwa wakizorotesha juhudi za Serikali katika mapambano hayo kwa kutozingatia kanuni za Afya, kutofuata na kutekeleza maelekezo ya wataalam wa Afya na hata kuzusha maneno yenye upotoshi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa katika kupambana na maradhi haya.
Ukweli ni kwamba hakuna Taifa lenye dhamira ya kuangamiza watu wake badala ya kuwalinda kwani ‘’hakuna Taifa bila watu na watu wenyewe ndio wanakigoma na watanzania kwa ujumla’’. Ifahamike kuwa, tafiti hufanyika na wataalam kujiridhisha kabla ya kukubali matumizi ya dawa au kutolewa kwa huduma mbalimbali za kiafya.
Kupanga ni kuchagua na tukichagua tusimame kwenye haki na kweli. Haitokuwa dhambi kuishukuru Serikali na watendaji wake kwa kuunga mkono juhudi mbalimbali za kutokomeza maambukizi ya Maralia ili kupunguza idadi ya vifo na athari nyingine zitokanazo na maradhi hayo katika Jamii zetu.
Sote tuzingatie kupima kabla ya kutumia dawa za Malaria kwani sio kila Homa ni Malaria, kutumia dozi ya maralia kwa ukamilifu na usahihi, kutumia chandarua chenye dawa, kupokea huduma ya unyunyiziaji wa kiuatilifu ukoko majumbani, wajawazito kuhudhuria Kliniki kwa wakati na kuharibu maeneo ya mazalia ya Mbu. Hapo ndipo tutaifanya Kigoma kuwa salama dhidi ya maambukizi ya Malaria.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa