Ikiwa ni Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 59 ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, Wananchi mkoani hapa wametakiwa kuendelea kutumia fursa ya uwepo wa maboresho makubwa ya Miundombinu ili kujiimarisha kiuchumi na kujiletea Maendeleo wao binafsi na mkoa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye alipozungumza na wakazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe Leo Aprili 26, 2023 kwenye Kilele cha Wiki ya Maadhimisho ya Muungano.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya Ujenzi wa Miundombinu pamoja na kuimarisha mifumo ya utoaji na upatikanaji wa Huduma za Jamii mkoani hapa kwa ajili ya Maendeleo ya Wananchi.
‘’Serikali inatekeleza Ujenzi wa Meli za uchukuzi wa watu na mizigo katika Ziwa Tanganyika pamoja na ukarabati wa Meli tatu zilizokuwa zikitumika awali, pia imeendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ikiwa ni pamoja na manunuzi ya mabehewa mapya 20 Treni ya Reli ya Kati na kuanza ujenzi wa Reli ya kisasa ya SGR’’
‘’Mkataba wa uboreshaji wa uwanja wa ndege wa Kigoma ulishasainiwa na kazi zikikamilika zitauwezesha uwanja kupokea ndege nyakati zote, kuhudumia abiria laki nne kwa Mwaka pamoja na kurefusha uwanja hadi kufikia Km 3’’ amesema.
Upande wa Nishati ya Umeme Andengenye amefafanua kuwa, Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa Umeme utakaoingiza kiasi cha Kv 400 kutoka Nyakanazi hadi Kidahwe, pamoja na miradi mingine miwili ambayo itauunganisha Mkoa na Gridi ya Umeme kutoka Tabora na Mpanda.
‘’Ongezeko la kiwango cha Umeme litawavutia wawekezaji hususani wanaotaka kuanzisha viwanda kutokana na hapo awali Mkoa kukosa Umeme wa kutosha na wenye uhakika hivyo kuunyima fursa ya uanzishwaji wa viwanda vikubwa na vidogo’’ ameongeza.
Aidha Mhe. Andengenye amewapongeza viongozi wakuu wa Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwaletea Maendeleo wananchi chini ya Muungano wa Serikali hizo mbili.
Pia Mkuu wa Mkoa ametumia fursa hiyo kuwaasa wakazi wa Wilaya ya Buhigwe kuutunza Mradi wa Maji ambao ameuwekea jiwe la Msingi kuelekea kilele cha Maadhimisho hayo uliopo katika kijiji cha Songambele wilayani humo.
Rai yangu kwenu, Mradi huu umeigharimu Serikali zaidi ya Shilingi Bil.1.6 hivyo hakikisheni mnaitunza miundombinu yake ili idumu na muweze kupata huduma hiyo kwa muda mrefu zaidi.
‘’Suala la kuchangia gharama za uendeshaji ni jambo la kawaida, hivyo ili kupata uendelevu wa huduma hii tunahitaji kulipia gharama za matumizi ya huduma ya maji ili kuwawezesha wasimamizi pamoja na kufanya manunuzi ya vifaa vinapoharibika’’ amesisitiza Andengenye.
Awali akiwasilisha Taarifa ya Ujenzi wa Mradi wa Maji kwa vijiji vya Buhigwe, Kavomo, Mlera na Bwega, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Buhigwe Mha. Gideon Katoto amesema mradi huo utakapokamilika unatarajia kunufaisha wakazi 14,378 wa vijiji hivyo.
Amefafanua kuwa Tanki lililojengwa linaujazo wa lita 500,000 huku chanzo cha Maji kikiwa na uwezo wa kuzalisha lita 1,994,500 kwa siku huku uhitaji wa Maji katika vijiji hivyo ukiwa ni lita 380,600 kwa Siku.
‘’Mradi huu kwa sasa umefikia Asilimia tisini na kazi zilizobaki za ulazaji wa mabomba ili kuwafikishia wananchi huduma inaendelea, aidha ukarabati wa matanki mawili katika vijiji vya Kavomo na Mulera umekamilika’’ amesisitiza Mhandisi Katoto.
PICHA ZA MATUKIO MBALIMBALI KATIKA MAADHIMISHO YA KIMKOA YA SHEREHE ZA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR WILAYANI BUHIGWE LEO APRILI 26, 2023.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa