Elimu ya Utunzaji wa Mazingira ikiambatana na uhiari wa wakazi wa mkoa wa Kigoma sambamba na kuitikia wito wa Kampeni ya Mti wa Mama katika utekelezaji wa zoezi la upandaji wa miti rafiki kwa mazingira itaufanya mkoa wetu kuwa eneo salama na la urithi sahihi kwa kizazi chetu kijacho.
Rasilimali ya Misitu ina umuhimu mkubwa katika suala la uhifadhi wa Mazingira hali kadhalika inakadiriwa kuchangia pato la Taifa kwa asilimia mbili hadi tatu. Aidha shughuli mbalimbali zimekuwa zikifanyika katika maeneo hayo huku zikithibitika kupunguza umasikini miongoni mwa wanajamii pia ikiwa ni chanzo kikuu cha nishati ya kupikia kwa asilimia 95.
Matumizi ya Nishati mbadala ikiwemo Gesi na Mkaa mbadala, kuitikia wito wa utunzaji wa misitu ikiwemo kuepuka ukataji wa miti ovyo, kulinda vyanzo vya Maji, kutovamia maeneo ya tengefu ya hifadhi za misitu, kulinda maeneo yenye uoto wa Asili pamoja na kuendesha kilimo na ufugaji wa kisasa ni kati aya mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa katika ulinzi wa maingira ya mkoa wa Kigoma na Tanzania kwa ujumla.
Ukataji wa miti midogo kwa jili ya kuni sambamba na uchomaji wa misitu hususani katika kipindi cha kiangazi na kuelekea msimu wa kuanza kwa shughuli za Kilimo katika maeneo mengi ya mkoa wa Kigoma ni ishara tosha ya kuelekea kulipokea jangwa na kupoteza sifa ya uwepo wa misitu mikubwa ya Asili na mvua za kutosha katika mkoa.
Hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kwa lengo la kudhibiti athari zinazotokana na uharibifu wa mazingira huku zikipuuzwa na baadhi ya wakazi sambamba na baadhi ya watendaji waliopewa dhamana kusimamia udhibiti wa shughuli za kibinadamu zinazoathiri misitu, uhifadhi wa mazingira na viumbe hai kwa ujumla.
Mfano ukifika katika Soko la wakulima Bugaga lililopo wilayani Kasulu, utashuhudia biashara ya kuni zinazotokana na miti midogo iliyopaswa kuachwa ili iweze kukua na kuendelea kuufanya mkoa kuwa salama kimazingira, zikiuzwa mafungu kwa mafungu kila siku ya Soko, hali inayoacha maswali yasiyo na majibu kuhusu mustakabali wa kutikia kwa ndoto ya kurejesha uoto wa asili ikiwemo miti ya asili.
Vizuizi vingi vya kudhibiti usafirishaji haramu au holela wa mazao ya misitu havina usimamizi thabiti unaozingatia nidhamu na miongozo ya serikali katika kuhakikisha rasilimali hizo zinalipiwa kwa usahihi au kutoza tozo ambazo zitawafanya wanaokiuka taratibu wahisi ni adhabu itakayowafanya wabadilishe mienendo ya kuchezea rasilimali zetu.
Vizuizi vyetu vinatenda kazi kwa kuzingatia mfumo wa pata nipate na kushindwa kuonesha nia ya dhati katika kudhibiti usafirishaji holela wa rasilimali hizo, japo hata makusanyo yanayopatikana bado hayatoshi kutekeleza zoezi la kurejesha kile kilichopotea huko msituni na katika maeneo ya hifadhi ambapo mamilioni ya miti yameendelea kuteketea kupitia kugeuzwa kuwa nishati.
Kwa mujibu wa Mwongozo endelevu wa Biashara ya Mazao ya Misitu yanayovunwa katika misitu ya Asili, unaotokana na Sera ya Taifa ya Mwaka 1998 wafanyabiashara wa Mazao ya misitu wa ndani na nje ya nchi wanatakiwa kufuata masharti na utaratibu ulioanishwa katika mwongozo huo.
Nukuu ‘’kuhusu manufaa ya vijiji vinavyopakana na misitu, mwongozo shirikishi wa misitu utazingatiwa kwa kutoa michango kwa vijiji ili vinufaike na rasilimali ya misitu. Vijiji vinavyopakana na misitu ya asili ya serikali vitanufaika kwa kuzingatia uendelezaji wa rasilimali za misitu na ufugaji nyuki pamoja na kuchangia mipango ya Maendeleo ya huduma za jamii kama vile shule na Zahanati’’
Suala hili ni kinyume katika maeneo mengi kwani uvunaji wa rasilimali hizi hufanyika kienyeji huku makusanyo yanayopatikana yakishindwa kuvifikia vijiji au maeneo lengwa ambayo mazao hayo yamevunwa na kusababisha kutotekelezeka kwa sera hiyo hali inayochangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira usio na urejeshi.
Hadithi ipi inafaa na inapaswa kusimuliwa kwa kizazi hiki kuhusu umuhimu wa kuwatunzia mazingira watoto wetu tunaohangaika kuwasomesha huku serikali ikiendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya kisasa ya kutolea huduma za jamii huku tukiandaa mazingira mabaya na hatarishi kwa kizazi hicho?
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ikishirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa, wakala wa Misitu nchini nchini (TFS) na wadau wa Mazingira, kwa Mwaka 2023 kwa pamoja mafanikio yaliyofikiwa ni kupandwa kwa miti 10,427,329 ili kukabiliana na janga hilo la kimazingira.
Aidha jumla ya vitalu 114 vya kuotesha miche ya miti vilianzishwa katika halmashauri nane za mkoa huku vikiwa na miche 5,893,732, Ikiwa rasilimali za hifadhi za misitu zilizopo ni Jumla ya hifadhi 6 kwa wilaya ya Buhigwe, 28 wilaya ya Kakonko, 35 wilaya ya Kasulu, mbili katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu, 37 Wilayani Kigoma, Sita katika Manispaa ya Kigoma Ujiji na Kumi wilayani Uvinza.
Ni hakika kuwa baadhi ya Kaya hutegemea kujipatia kipato cha kujikimu kimaisha kupitia biashara haramu ya rasilimali hizi za misitu bila kujua kuwa wanachokifanya ni kinyume na Sheria kupitia biashara ya mkaa, kuni na hata uchimbaji wa mizizi na matumizi ya magome ya miti kwa ajili ya tiba asili.
Ni jukumu la kila mwananchi kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha tunarejesha uoto wa asili ilkiwemo upandaji wa miti rafiki kwa mazingira, kutunza maeneo tengefu ya misitu ya vijiji, kuwajibika kwa kuepuka na kudhibiti utoroshwaji wa maliasili zetu sambamba na kushiriki mazoezi ya upandaji wa miti na kuitunza.
Shime kwa wanakigoma tunapopewa miti ya bure na serikali kwa ajili ya kuipanda, tukatekeleze jambo hilo kwa moyo mkunjufu, tuepuke kuwaficha wahalifu wanaovamia maeneo ya hifadhi za misitu kwa maslahi yao binafsi, tuungane na taasisi za Umma na zile binafsi katika kusimamia uhifadhi wa mazingira pamoja na kila mmoja kushiriki katika ulinzi wa mazingira.
Ikumbukwe kwa sasa misitu iliyopo mkoani Kigoma inaelekea kuwa lulu kutokaka na kuibuka kwa biashara halali isiyohitaji jasho ya hewa ukaa. Uwezo wetu wa kuingia katika biashara hiyo ni sifa tosha kuwa tupo katika dunia salama kimazingira pamoja na changamoto tulizonazo za uharibifu wa mazingira.
Ni jukumu la kila mmoja kuutafakari ulimwengu ujao huku tukifikiria kwa kina kuhusu maisha ya vizazi vijavyo.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa