Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye (kushoto) akimsikiliza Meya wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Mhe. Baraka Lupoli (katikati) aliposhiriki Mkutano wa Baraza la Madiwani katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji kwa ajili ya kupikea na kujadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Juni 30, 2022. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kigoma/Ujiji Athumani Msabila.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amepiga marufuku Halmashauri zote mkoani Kigoma kutumia mifumo tofauti na ule wa TAUSI katika kufanya makusanyo ya ndani kwenye Halmashauri hizo.
Andengenye ametoa Maelekezo hayo Juni 6, 2023 wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Madiwani Manispaa ya Kigoma/Ujiji kujadili Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha unaoishia Juni 30, 2022.
Mkuu wa Mkoa amesema kitendo cha kutumia mifumo ya zamani ya ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri ikiwa ni pamoja na matumizi ya Risiti kinaendelea kutoa mianya ya kufanyika kwa urasimu kwa baadhi ya watendaji wasio waaminifu.
‘’Kupitia Baraza hili ninatoa Maagizo kuwa ni marufuku kwa watendaji katika Halmashauri zote mkoani hapa kutumia au kuidhinisha matumizi ya mifumo tofauti na huu uliorasimishwa na Serikali katika kukusanya mapato ya ndani na watakao kaidi na kwenda kinyume watakuwa wanakiuka Maelekezo ya Serikali kwa makusudi na hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao’’ amesema.
Ameongeza kuwa, mfumo wa Tausi unawafanya wananchi kuwa na Imani kuwa malipo wanayoyafanya yanakwenda sehemu sahihi badala ya baadhi ya watu kutunza Fedha za Serikali kwenye mifuko yao na kuziwasilisha kwa muda wanaotaka.
Akitoa maelekezo kuhusu utekelezaji wa Taarifa ya Mkaguzi wa ndani kwa Halmashauri hiyo, Mkuu wa Mkoa amesisitiza Baraza hilo la Madiwani kwa kushirikiana na watendaji wa Halmashauri kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi watakaobainika kuhusika na vitendo vya ubadhirifu na kusababisha Manispaa hiyo kukosa mapato kama ilivyokusudiwa.
‘’Nasisitiza uchukuaji wa hatua uhusishe watumishi wote wenye ajira za kudumu na wale wenye mikataba ili kuimarisha uwajibikaji kwenye usimamizi wa Fedha na Rasilimai nyinginezo za Serikali ili kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato’’ amesisitiza Andengenye.
Pia kiongozi huyo amewataka Madiwani katika Halmashauri zote mkoani hapa kuzingatia kanuni za Maadili ya Utumishi wa Umma katika utendaji kazi wao.
‘’Epukeni matumizi mabaya ya Madaraka kupitia nafasi zenu, hii itawasaidia wananchi kuwaamini katika maamuzi mnayoyafanya na kuondoa malalamiko yasiyo na msingi katika jamii mnayoiongoza’’ ameshauri Andengenye.
Naye Meya wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Baraka Lupoli amesema upungufu wa watumishi katika Idara ya Fedha na Biashara katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji unachangia kwa kiasi kikubwa kupotea kwa mapato ya ndani hali inayosababaisha makusanyo kukusanywa chini ya kiwango.
‘’Makadirio ya makusanyo yetu kwa Mwezi ni zaidi ya Shilingi Mil. 400 ila kutokana na changamoto hizo, makusanyo yetu hushuka hadi kufikia kiasi cha Shilingi Mil. 270 kwa Mwezi’’ amesisitiza Mhe. Meya.
Kwa upande wao Madiwani wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji wameiomba Serikali kutafuta suluhisho la changamoto ya uhaba wa watumishi katika Idara ya Fedha na Biashara ili kuongeza tija na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.
Upungufu wa watumishi kwa sasa umesababisha Halmashauri hiyo kutumia wakusanya mapato wenye Ajira za mikataba ambao baadhi yao wamekosa uaminifu na kusababisha upotevu mkubwa wa mapato katika Halmashauri hiyo.
Kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji imepata Hati Safi ya ukaguzi wa Hesabu za Serikali.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa