Wakuu wa Taasisi za Serikali zinazotekeleza Miradi ya Barabara mkoani Kigoma wametakiwa kujenga tabia ya kutoa taarifa za miradi wanayoisimamia na kuitekeleza kwa ili wananchi wawe na uelewa kuhusu kazi zinazofanywa na Serikali pamoja na kuwajengea uwezo wa kufuatilia na kuhoji kuhusu kazi hizo.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mhe. Thobias Andengenye alipokuwa akifungua kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa kilichofanyika leo Tarehe 14 Desemba 2022 katika Ukumbi wa NSFF Manispaa ya Kigoma/Ujiji.
‘’Kupitia viongozi wa ngazi mbalimbali za kisiasa, tunaweza kufikisha ujumbe kwa Wananchi ili waweze kufahamu kiasi cha Fedha kinachotolewa na Serikali kisha kuelekezwa kwenye Miradi ya Barabara. Pia wataweza kutambua aina ya Miradi inayotekelezwa pamoja na hatua zilizofikiwa. Hii itawaongezea ufahamu kujua miradi inayotekelezwa na kuondoa maswali yasiyo ya lazima’’ alisema.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa matengenezo ya barabara 2021/2022 na 2022/2023, Miradi ya maendeleo na ahadi za viongozi, Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa Mha. Narcis Choma amesema mtandao wa Barabara unaohudumiwa na wakala huyo kimkoa unajumla ya Kilomita 1,547.03 ambapo Barabara kuu ni Km. 753.63 na Barabara za Wilaya ni 135.5.
Amefafanua kuwa, upande wa Madaraja wanahudumia Jumla ya madaraja 381 yaliyopo barabara kuu yakiwa 130 na za Mkoa 251. Aidha amesema matarajio ni kuongeza utoaji wa huduma za barabara na madaraja kuendana na upatikanaji wa Fedha ili kuondoa kero hiyo kwa wananchi.
Upande wake meneja wa Wakala wa Barabara za vijijini na Mjini Mkoa Mha. Godwin S. Mpinzile, amesema wataendelea kuzibainisha na kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali za barabara ili kuhakikisha maeneo mengi ya Mkoa yanapitika na kufikika kwa urahisi.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa