Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thibias Andengenye amefungua Mkutano wa kupokea maoni kwa ajili ya kuhuisha Sera ya Taifa ya Uchukuzi ya Mwaka 2003 na kutoa wito kwa washiriki wa mkutano huo kutoa maoni yenye kujikita katika mapendekezo yatakayolenga kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma katika sekta hiyo ili kutatua changamoto zilizopo na zinazotarajiwa kuwepo kwa lengo la kuchochea Maendeleo enedelevu ya mkoa na Taifa kwa ujumla.
Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo alipozungumza wakati akifungua kikao hicho, ambapo amewakumbusha washiriki kutambua kuwa serikali imeamua kutekeleza zoezi hilo ili kubaini mahitaji halisi ya huduma kupitia Sekta hiyo, kuendana na maoni ya wananchi wenyewe kwa kuwafikia katika maeneo yao.
Mkuu wa Mkoa ameipongeza Serikali ya awamu ya Sita kwa kubaini mapungufu yaliyomo kwenye sera hiyo na kuchukua hatua madhubuti kwa kutoa fursa kwa wananchi kuchangia mawazo yao katika uboreshaji wake kwani imekuwa ikichangia kukwamisha maendeleo endelevu ya Taifa.
Upande wake Mkurugenzi wa ufuatiliaji na Tathimini kutoka Wizara ya Uchukuzi Bi. Devotha Gabriel amesema Wizara ya Uchukuzi imekuwa ikifanya mapitio ya miongozo yake ili iweze kuendana na mahitaji halisi ya wananchi ikiwemo na kuamua kupitia Sera ambazo haziendani na mabadiliko ya kimaendeleo yaliyopo sasa hivyo kuwa nyuma ya wakati na kutokidhi matakwa ya wananchi katika kupata huduma.
Amesema endapo sera hiyo itakamilika itaweka mwongozo utakaochochea mfumo wa utoaji huduma za uchukuzi nchini na kuongeza pato la wananchi, mkoa na Taifa kwa ujumla.
Niwasihi washiriki wote, maoni mnayoyatoa ni kwa niaba ya watanzani wengi ambao hawajafika hapa, hivyo niwaombe mtangulize maslahi ya taifa katika kutoa ushauri, maoni na mapendekezo yenu’’ amesisitiza Devotha.
Mkutano huo umehudhuriwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Elisante Mbwilo, wakurugenzi wa Wizara ya Uchukuzi, Mshauri Elekezi (TALANTA) Wataalam kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma pamoja na wadau mbalimbali kutoka Sekta za Umma na binafsi.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa