Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) limekabidhi Hadubini Tano zenye Thamani ya Shilingi Mil. 35 kwa ajili ya kuimarisha Huduma za uchunguzi wa kimaabara katika Vituo vinavyotoa Huduma ya Upimaji wa Ugonjwa wa Kifua Kikuu mkoani Kigoma.
Mara baada ya Kupokea Hadubini hizo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Leba amelishukuru Shirika la THPS na kusisitiza kuw,a vitendea kazi hivyo vitapanua wigo wa Matibabu ya Maradhi ya Kifua Kikuu mkoani Kigoma.
Dkt. Leba amesema vifaa hivyo vitaongeza kiwango cha ugunduzi wa Magonjwa ya kifua Kikuu pamoja na kusaidia kutambuliwa kwa wagonjwa katika hatua za awali na kuruhusu kuanza matibabu ya mapema kabla ya kuathirika zaidi.
‘’Tunawashukuru THPS kwani ufadhi wa vitendea kazi hivi ambavyo vitaongeza Idadi ya vituo vya kupimia wagonjwa pamoja na kusogeza huduma hii muhimu karibu na Wananchi’’ amesema Dkt. Leba.
Naye Meneja wa Kanda wa Mradi wa THPS Dkt. Benedict Nyilo, amesema Hadubini hizo zitagawiwa katika vituo vitano vya Uchunguzi wa Kifua kikuu kwenye Halmashauri za Wilaya Kakonko, Kasulu, Uvinza na Manispaa ya Kigoma/Ujiji.
‘’Tunatambua na kuthamini Dhamira ya Serikali katika kukabiliana na kutokomeza kabisa ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini ifikapo Mwaka 2030, hivyo tumetoa vifaa hivi kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuukabili ugonjwa huo’’ amesema Dkt. Nyilo.
Dkt. Nyilo amewataka Wananchi kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupima Afya zao wanapobaini dalili za ugonjwa huo, kwani vipimo vinatolewa bure ikiwa ni mkakati wa Serikali katika kuyakabili maradhi hayo.
Naye Mtaalam kutoka Maabara Kuu ya kudhibiti Maradhi ya Kifua Kikuu na Ukoma ya Jijini Dar es Salaam, Said Mfaume, amesema hadubini hizo zitaongeza kasi katika uibuaji wagonjwa wapya wa Kifua Kikuu mkoani Kigoma.
Ameendelea kusisitiza kuwa, kupatikana na Hadubini hizo kutaongeza Idadi ya Vituo vya kutolea Huduma za Upimaji wa ugonjwa wa Kifua Kikuu mkoani Kigoma na kuifikia idadi kubwa ya walengwa katika kupambana na ugonjwa huo.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa