Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mhe. Thobias Andengenye ameupongeza Uongozi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kusimamia shughuli za bandari kwa ufanisi jambo linaloendelea kuimarisha usalama na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Andengenye ametoa pongezi hizo alipotembelewa na Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Kigoma, Adam Mamilo aliyefika ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa lengo la kujitambulisha mara baada kuwasili katika kituo chake kipya cha kazi Mkoani hapa.
Amesema TASAC inapaswa kuongeza nguvu katika kuboresha huduma za usafirishaji majini hususani katika bandari ya Kigoma kutokana kasi ya serikali kufanya maboresho makubwa ya miundombinu mkoani hapa, hali inayovutia wafanyabiashara wengi kutoka ndani na nchi jirani za Burundi, Kongo DR na Zambia kutumia bandari hiyo.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa amesema fursa za kiuchumi zitokanazo na Ziwa Tanganyika zimechangia ongezeko kubwa la vyombo vya uchukuzi visivyo rasmi vinavyochangia kuhatarisha usalama wa wananchi wanaovitumia, hivyo serikali kwa kuliona hilo imeamua kuwekeza katika uboreshaji miundombinu ya uchukuzi ikiwemo ukarabati wa Meli ya Mt. Sangara, Mv Liemba pamoja na Mv. Mwongozo.
"Nitoe Rai kwa uongozi wa TASAC mkoa wa Kigoma kwenda kusimamia na kuhakikisha ukarabati wa meli hizo unakamilika kwa wakati ili tuweze kukabiliana na mahitaji makubwa ya usafirishaji wa watu na bidhaa za kibiashara huku tukiimarisha usalama wa maisha ya watu na mali zao katika ziwa Tanganyika" amesema.
"Kwa sasa tayari mkoa umeunganishwa na Bararara ya Lami kutoka Kigoma kwenda mikoa ya Kagera na Shinyanga huku upande wa Tabora ujenzi ukiwa katika hatua za mwisho na kwa upande wa Katavi ujenzi unaendelea vizuri, hii inazidi kuchangia ongezeko la wawekezaji ambao pia watatumia bandari kusafirisha bidhaa na kuongeza mzigo wa utendaji kazi wa bandari ya Kigoma" ameeleza Rugwa.
Upande wake Afisa Mfawidhi wa TASAC Kigoma Adam Mamilo ameahidi kushirikiana na viongozi wa Serikali ya Mkoa kwa ajili ya kupokea ushauri utakaolenga kuhakikisha miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi wa Bandari inakamilika kwa wakati.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa