Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye ameuelekeza Uongozi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) Mkoa wa Kigoma kuchukua hatua za kisheria dhidi Taasisi au mtu yoyote anayetekeleza shughuli za kibinaadamu katika maeneo tengefu ya Hifadhi za Barabara ili kuruhusu yaweze kutumika kama ilivyokusudiwa na Serikali.
Mkuu wa Mkoa ametoa maelekezo hayo kufuatia athari zinazoendelea kujitokeza kutokana na baadhi ya wakazi kuvamia Hifadhi za barabara na kufanya shughuli mbalimbali za kibiashara, Kilimo, kuchunga mifugo pamoja na uchimbaji wa mchanga hali inayosababisha uharibifu wa miundo mbinu hiyo.
‘’Serikali inatumia kiasi kikubwa cha fedha kuboresha miundombinu hii muhimu ya usafirishaji lakini baadhi ya watu wamevamia na kuanzisha Karakana kwa ajili ya kutengeneza magari na pikipiki, ujenzi wa vibanda vya Biashara, kufanya shughuli za kilimo, pamoja na uchimbaji wa mchanga hususani nyakati za mvua au katika maeneo yenye madaraja’’ amesema.
Pamoja na shughuli hizo kuathiri barabara na kusababisha msongamano kwa baadhi ya maeneo, Andengenye ametoa Tahadhari ya uwezekano wa kutokea vifo au majeruhi kwa watu wanaovamia hifadhi hizo kutokana na ajali zinazoweza kusababishwa na vyombo vya usafiri kuacha njia na kuwafikia kwa wepesi.
‘’Hatukatazi watu kutafuta riziki lakini pia utafutaji huo uende sambamba na uzingatiaji wa Sheria za nchi na Usalama wetu, kwani Serikali ilishatenga maeneo rasmi kwa ajili ya shughuli za kibiashara lakini baadhi ya watu wanaamua kupuuza kwa makusudi na kuendelea kuendesha shughuli za kiuchumi katika maeneo yasiyo sahihi’’ Amefafanua Andengenye.
Aidha Andengenye amesisitiza kuwa, maboresho makubwa ya Miundombinu ya Barabara yanayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita yaende Sambamba na muitikio wa wananchi katika kujiimarisha kiuchumi ili kukabiliana na wimbi kubwa la wawekezaji kutoka nje ya Mkoa wa Kigoma wanaoanza kuzitazama na kuchangamkia fursa zilizopo kufuatia mkoa kuzidi kufunguka kibiashara.
‘’Uwepo wa Miundombinu rafiki ya uchukuzi na usafirishaji pamoja na Serikali kuendelea kuuimarisha hali ya utoshelevu wa Umeme , vitaongeza kasi ya uwekezaji na ushindani wa kibiashara sokoni kutoka kwa wawekezaji mbalimbali wa nje ya Mkoa, hivyo sisi wenyeji tunapaswa kuwa wa kwanza kuchangamkoa fursa zilizopo’’ amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
Upande wake Meneja wa TARURA Wilaya ya Kigoma Mha. Elias Mutapima amesema changamoto wakazi kufanya uharibifu mkubwa wa mitaro, kutupa taka ovyo zinazosababisha mitaro kuziba na hata kupasuka pamoja na kushusha vifaa vya ujenzi katika maeneo ya barabara.
Ameendelea kueleza kuwa, matumizi mabaya ya hifadhi za Barabara katika uwekaji wa miundombinu mingine kama ile ya Umeme na Maji vimeendelea kusababaisha kuchelewa kukamishwa kwa baadhi ya miradi na kuendelea kuwepo kwa adha ya ukosefu wa barabara zenye ubora katika baadhi ya Maeneo katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji.
''Ili kukabiliana na Changamoto hizi, tunajitahidi kujenga mitaro na makaravati ili kudhibiti Barabara zisiharibiwe na Maji ya Mvua, kuendelea kutoa Elimu ya utunzaji wa Barabara pamoja na kushirikiana na wataalam wenzetu ili kuhakikisha tunahamisha kwa haraka miundombinu iliyowekwa kwa makosa kwa lengo la kuharakisha ufikishaji wa huduma kwa Wananchi'' ameeleza Mha. Mutapima.
PICHA; Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye (Kushoto) akipokea na kupitia taarifa ya utekelezaji wa Ujenzi wa miradi ya Barabara zinazosimamiwa na TARURA katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji, kutoka kwa Meneja wa TARURA Wilaya ya Kigoma Mha. Elias Mutapima(Kulia)
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye akiburudika na kinywaji aina ya Kahawa huku akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza alipotembelea wilaya hiyo kwa lengo la kukagua utekelezaji wa Ujaenzi wa Miradi ya Barabara zilizo chini ya TARURA.
PICHA: Muonekano wa Baadhi ya Barabara zilizotembelewa na Mkuu wa Mkoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza pamoja na Manispaa ya Kigoma/Ujiji
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye akizungumza na wakazi wa Kata ya Mwandiga katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji akiwa katika ziara yake ya kukagua Miradi ya Ujenzi wa Barabara.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa