Kamati za Maafa kutoka Mkoa wa Kigoma pamoja na mikoa ya Kivu Kusini na Tanganyika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimekutana kwa lengo la kubadilishana mbinu, kujadili na kuweka mikakati ya pamoja yenye lengo la kukimarisha njia za kukabiliana na majanga katika ukanda huo.
Akifungua Mkutano uliozikutanisha pande hizo na kufanyika tarehe 20-21, Februari 2024 katika Ukumbi wa NSSF Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mkuu wa Mkoa wa KigomaThobias Andengenye amesema athari za majanga huwa hazina mipaka kijiografia hivyo ni jambo jema kwa pande hizo kukaa chini na kuweka mikakati ya pamoja yenye lengo la kuepuka au kupunguza athari zinazoweza kuyakumba maeneo hayo na kuleta madhara kwa wakazi.
Ameyataja majanga yanayoendelea kuleta athari mara kwa mara katika maeneo hayo kuwa ni ukosefu wa Amani, uwepo wa magonjwa ya mlipuko, ongezeko la wakimbizi, uharibifu wa mazingira, mafuriko, kuongezeka kwa kina katika ziwa Tanganyika pamoja na uwepo wa ajali za marakwa mara katika ziwa hilo.
Kupitia kikao hicho, mkuu huyo wa mkoa amezitaka Kamati hizo kuhakikisha zinaweka mikakati ya kudumu katika kushughulikia majanga hayo ili kupunguza athari ikiwemo vifo, ukosefu wa Amani katika nchi ya Congo unaochangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira pamoja na mdororo wa kiuchumi katika ukanda huo.
Upande wake Mratibu wa Shirika lisilo la kiserikali la REDESO Mkoa wa Kigoma Emmanuel Solomon amesema kamati hizo zinakabiliwa na changamoto za udhaifu kwenye usimamizi wa Sheria na miongozo inayotungwa na nchi husika za Tanzania na Congo DR.
Amezitaja changamoto nyingine kuwa ni ongezeko la wahamiaji haramu kutoka nchi ya Congo na kuingia Tanzania kinyume cha Sheria, ufinyu wa bajeti kwa ajili ya kuziwezesha kamati hizo kufanya ufuatiliaji sambamba na uelewa mdogo wa wakazi katika maeneo hayo kuhusu athari za majanga ili kushiriki kuchukua tahadhari.
Solomon amesema baadhi ya mapendekezo ya jumla waliyoyafikia kupitia kikao hicho ni pamoja na kuzitaka Serikali za pande zote mbili kutilia mkazo na kufuatilia kwa karibu mikakati ya kukabiliana na majanga, kuhakikisha mikakati hiyo inatekelezwa kwa vitendo sambamba na kuziwezesha kamati kifedha ili zimudu kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Akifunga Mkutano huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kanali Michael Ngayalina ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe ametoa wito kwa Kamati hizo kushirikiana na mamlaka husika za serikali zao ili kuchukua hatua za muda mrefu katika kukabiliana na majanga.
Aidha Kanali Ngayalina amewashukur wadau wote waliofanikisha kufanyika kwa Mkutano huo na kusisitiza kuwasisitiza wajumbe kuhakikisha maazimio yaliyofikiwa yanafanyiwa kazi kwa ufasaha.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa