Serikali mkoani Kigoma imeahidi kuendelea kushirikiana na mikoa jiraji inayopakana na mkoa huo katika nchi ya Burundi kwa lengo la kukabiliana na kupunguza athari za majanga ikiwemo uharibifu wa Mazingira, Mali pamoja na kusababisha vifo.
Mkuu wa Wilaya ya Kibondo Kanali Agrey Magwaza ametoa Kauli hiyo alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kwenye Mkutano ulioikutanisha Kamati yay a Maafa ya Mkoa wa Kigoma na zile za mikoa ya nchi hiyo jirani kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya pamoja kwa ajili ya kukabiliana na majanga katika maeneo hayo.
Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu huyo wa wilaya amewataka wajumbe wa mkutano huo kubainisha kwa uwazi majanga yanayozikabili jamii katika mikoa lengwa ili kujadili na kuweka mikakati ya pamoja kwa ajili ya kubaini viashiria na kubadilishana uzoefu wa namna ya kuyakabili majanga sambamba na kuijengea jamii uwezo katika kuchukua tahadhari.
Mwakilishi wa Kamati ya Maafa kutoka nchini Burundi David Minteretse amesema kikao hicho ni sehemu ya suluhisho muhimu katika kukabili maafa yatokanayo na majanga mbalimbali kwani kila upande utafahamu jukumu lake katika kukabili majanga yanapotokea.
Jamii inapaswa kufahamu kuwa majanga hayana mipaka ya kibinaadamu hivyo pande zote zinapaswa kujijengea utayari kifedha, kielimu sambamba na kiteknolojia ili kuzuia madhara au kupunguza athari zake’’ amesema mwakilishi huyo.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Help Age Tawi la Kibondo, Yovitha Mrina amesema kupitia mkutano hupo, wanatarajia kuweka mikakati madhubuti ili kujenga utayari kwa wananchi wa maeneo hayo kwa ajili ya kukabili majanga sambamba na utunzaji wa Mazingira.
Mapema mwezi Februari 2024, Kamati ya kukabiliana na majanga mkoa wa Kigoma ilikutana na Kamati kutoka nchi ya Congo DR kwa lengo la kujadili changamoto hizo ambapo nchi hizo mbili zilikubaliana na kuweka mikakati kadhaa ikiwa ni pamoja na kudhibiti uharibifu wa Mazingira katika Ziwa Tanganyika.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa