MKUU WA MKOA WA KIGOMA MHE. THOBIAS ANDENGENYE AKIZUNGUMZA WAKATI AKIFUNGUA MKUTANO ULIOWAKUTANISHA WADAU WA KIKODI MKOANI KIGOMA PAMOJA NA TUME YA RAIS YA MABORESHO YA KODI ULIOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA KIGOMA SOCIAL HALL, MANISPAA YA KIGOMA UJIJI JANUARI 22, 2025
Wafanyabiashara mkoani Kigoma wametakiwa kutumia fursa ya Mkutano unaowakutanisha na Tume ya Rais ya Maboresho ya kodi kuwasilisha changamoto zao za kikodi na kupata ufumbuzi kutoka kwenye tume hiyo ili kuendelea kuimarisha mifumo sahihi ya ulipaji kikodi kwa maendeleeo ya Taifa.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye ametoa kauli hiyo alipofungua kikao kilichowakutanisha wadau wa kodi mkoani Kigoma na Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi kilichofanyika mkoani hapa na kuwataka wafanyabiashara hao kueleza kero zao na kupendekeza namna bora ya kuzipatia utatuzi bila kuathiri biashara zao na mfumo wa ukusanyaji kodi.
Amesema Mhe. Rais ameanzisha tume hiyo ili kuzigusa kuzibaini na kuzifanyia kazi changamoto za wafanyabiashara kwa kuwafikia katika maeneo yao, kupokea changamoto pamoja na kutoa ushauri na kutatua masuala yote yanayotatiza ukusanyaji wa kodi kwa maendeleo ya Taifa.
Awali akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Tume, Mwenyekiti wa Tume hiyo Balozi Maimuna Tarishi amesema lengo la tume ni kupokea maboresho ya ukusanyaji kodi yanayotekelezeka na kuongeza fursa za upatikanaji wa kodi kwa njia rahisi na rafiki.
Amesema tume hiyo inazunguuka katika mikoa yote ya Tanzania bara na Zanzibar ili kukutana na wafanyabiashara kutoka Sekta za Umma na zile binafsi ili kutatua kero za kikodi na kudumisha mazingira rafiki baina ya taasisi hizo na sekta yenye jukumu la kukusanya mapato.
Upande wake mjumbe wa Tume hiyo Prof. Mussa Asad amesema kupitia mikutano yao na wadau wa kodi, wanajadili kuhusu kubaini maeneo yanayostahili kufikiwa kikodi lakini hayafikiwi wakati yakiwa na kumbukumbu nzuri za uzalishaji, kufuatilia hali ya ushughulikiwaji wa malalamiko ya kikodi, kutambua wadau wa kodi walipo pamoja na kero mbalimbali za utozaji kodi wanazokabiliana nazo wananchi na ambazo wasingependa kuziona zikiendelea.
Mkutano huo umeikutanisha tume hiyo na wataalam kutoka Sehemu ya Viwanda, Biashara na uwekezaji kutoka Sekretariet ya Mkoa, wakurugenzi watendaji wa Halmashauri, wakuu wa Taasisi mbalimbali, wafanyabiashara wakubwa, wati na wajasiriamali wadogo.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa