Kila uchao Idadi yetu inaongezeka hali kadhalika uwepo wa ongezeko la mahitaji. Kwa mujibu wa Taakwimu za matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi kwa Mwaka 2012 Mgawanyo wa Idadi ya Watu kwa Mkoa wa Kigoma ilikuwa Mil 2.2 ambapo kwa matokeo ya Awali ya Sensa ya Watu na Makazi kwa Mwaka 2022, idadi imeongezeka hadi kufikia Mil. 2.5
Ongezeko hilo linamaanisha pia kuongeeka kwa mahitaji ya Jamii katika matumizi ya Utajiri wetu wa Asili, hali inayosababisha baadhi yetu kujikita katika maeneo ya mashambani au maporini kwa lengo la kujitafutia mkate wa kila uchao. Kwangu mimi ni Jambo jema bali hugeuka dhambi pale tunapokiuka Sheria za ulinzi wa Rasilimali hizo kwa kuvamia na kuharibu urithi wetu wa asili katika mazingira lindwa na hata yale yaliyoidhinishwa kufanyika kwa shughuli za kibinaadamu.
Ifahamike kuwa, Rasilimali asili ni Maliasili ambazo hupatikana katika Mazingira Asilia bila hitaji la kuchakatwa na Binadamu na hutumika kukidhi mahitaji ya viumbe hai mbalimbali pamoja na mwanadamu, ambaye katika hali ya kustaajabisha yeye ndiye mnufaika mkubwa wa rasilimali hizo na ndiye anayeongoza kwa uharibifu kutokana na kupitiliza au kukosa usahihi wa matumizi.
Napata kigugumizi kuamini kuwa ni kwa kiasi gani mahitaji yetu yanatusukuma kwenye shida nyingine kubwa ya Athari za uharibifu wa mazingira pamoja na uvunjifu wa Sheria huku tunaona makatazo na maonyo mbele yetu na tunajua madhara yatakayoweza kujitokeza siku zijazo. Kuvunja Sheria za uhifaddhiwa Mazingira ni sawa na kuvunja mlango wa nyumba tunayoishi wenyewe bila kujali nini kitakachotokea usiku wa manane.
Leo maeneo mengi ya hifadhi yameendelea kuvamiwa na kuharibiwa vibaya huku wavamizi wakienda mbali zaidi kwa kuhujumu mali na uhai wa watu wanaojaribu kurejesha mazingira yaliyoathiriwa katika hali yake ya awali kwa maslahi ya wachache. Hakuna uadilifu hapa huu ni uhalifu mkubwa kwani athari zake ni za sasa, kesho na kesho kutwa lazima ukemewe na hatuazichukuliwe.
Nilipata bahati ya kuzungumza na wakazi, Jamii ya wafugaji pamoja na wakulima ambao wamekumbushwa na Serikali kutambua mipaka yao halisi ya Ardhi kwa ajili ya shughuli za kibinaadamu dhidi ya zile za uhifadhi wa Mazingira. Haiingii akilini kuamini kwamba mtu mzima anaamini bora yeye atekeleze malengo yake na sio kulinda mazingira kwa maslahi ya kizazi hiki na kijacho.
Mkoa wa Kigoma tukiwa na Urithi wetu wa Asili wa Hifadhi za Misitu, Hifadhi za Wanyama, Mto Malagarasi na Ziwa Tanganyika, kwa jicho la mazoea hakuna tunachodhani kinatufaa sasa na baadae? Hivi mpaka manabii wanaotembea akina Mfalme mwana wa Emir na wafuasi wake wasimame na kutuhubiria kuhusu mazingira? Au tushikiwe fimbo za wazungu na walinzi wetu wa Misitu ndipo akili huturejea na kuamini kuwa tunajikosea?
Hatuoni mpaka tuonyeshwe wakati faida zitokanazo na rasilimali hizo asilia ni kwa ajili yetu wenyewe? Hapa sio bure tujitafakari na kujiuliza hizi mvua zilizopoteza majira nini chanzo chake? Je tuko tayari kuigeuza Kigoma ya Kijani kuwa jangwa? Tunautayari wa kuipoteza mito yetu inayotusaidia kulima mazao nyakati zote huku ikitupa vitoweo vya Samaki watamu maarufu kama Kuhe,nguruka,migebuka na vilamba mawe wa pale Uvinza? Wapi wanyama wetu watatii kiu zao? Hayo yote yako mikononi mwetu na waamuzi wa ustawi wa viumbehai hao ni sisi.
Mwanafalsafa Rabindranath Tagore aliwahi kusema ‘‘Yule anayepanda Mti hanauhakika wa kukaa chini ya kivuli cha mti huo, bali kwa kiasi Fulani anakuwa na uelewa wa nini maana ya maisha’’. Muhenga huyu aliona mbali na kubaini ni kwa namna gani hatuitazami kesho yetu kwa upande wa Mazingira.
Pamoja na uwepo wa changamoto kubwa za kimazingira katika Eneo la Bonde la Ziwa Tanganyika ambalo kitaalam linajumuisha Mikoa ya Shinyanga, Tabora, Katavi, Rukwa, Singida, Geita na Kigoma yenyewe, bado tunanafasi kubwa ya kufanyia kazi nafasi yetu na kuyafanya maeneo hayo ya vyanzo vya maji, kuendelea kuwa salama ili yaweze kudumu kwa maslahi ya kimazingira na urithi wa jamii yetu.
Mtaalam wa mazingira Mhandisi Odemba Cornel(LTBWB), anasema ‘‘Dunia ina mfumo na tabia za viumbe hai kwani yanapotokea mabadiliko yanayokinzana na uasili wake nayo huenenda tofauti na vile ambavyo tumeizoea’’ Anatoa mfano kuwa, tunapofanya shughuli za kibinaadamu katika maeneo owevu tunaziba njia za ufyonzaji wa Maji kwenda chini ya ardhi na kusababisha uwezekano mkubwa wa maji kutuama kwa muda mrefu au kutokea mafuriko maeneo ya upande wa chini wa mito mvua inaponyesha kwa wingi.
Ni mapema mno kukiri kuwa jukumu la kuendeleza na kulinda Rasilimali Asili zetu na Mazingira yake libaki kwa Serikali pamoja na wadau wa mazingira wakati wanufaika tupo na wanaoharibu kesho yetu ni sisi wenyewe hali kadhalika tunaoendelea kupata madhara ya matendo yetu pia ni sisi wenyewe.
Kwa sababu tumezoea kusimamiwa basi tujikumbushe kuhusu uwepo wa Sheria za usimamizi wa Mazingira kama vile hifadhi za vyanzo vya Maji, hifadhi za Bioanuai mahali asilia na pasipo asilia, usimamizi wa rasilimali Misitu, hifadhi ya rasilimali uvuvi na wanyamapori nk, ili tutakapowajibishwa tusijemtwika mtu lawama.
Kabla ya kusubiri kuwajibishwa na Sheria za Usimamizi wa Mazingira, tuguswe na kuamini kwamba Dunia tuliikuta na imekuwa mahali salama kwetu kuishi, basi pamoja na heka heka za kujiinua kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali za maendeleo, tujue tutapita. Hivyo tuifanye iwe sehemu salama pia kwa vizazi vyetu wasije wakayatia bakora makaburi yetu na kuona jinsi watangulizi wao tulivyoizima haki yao kwa ajili ya ubinafsi wetu.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa