SHUGHULI ZA KIBINADAMU KARIBU NA BARABARA ZASABABISHA UCHAKAVU WA MIUNDOMBINU
Posted on: October 12th, 2017
Shughuli za kibinadamu, wizi wa vyuma kwenye makaravati na alama za barabarani, utitiri wa vizuizi barabarani, upitishaji holela wa mifugo, magari kuzidisha uzito unaotakiwa na utupaji wa taka kwenye mitaro yabarabara; vimetajwa kuwa vyanzo vikubwa vya uharibifu na uchakavu wa miundomvinu ya barabara.
Haya yameelezwa katika kikao cha kwanza cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Kigoma kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Aidha tatizo jingine limekuwa la wananchi kuongeza ujenzi kwenye hifadhi ya barabara, kuweka miundombinu ya biashara sehemu za barabara kinyume na sheria.
Kufuatia hali hii Meneja wa Wakala wa barabara Mkoa wa Kigoma Mhandisi Narcis Choma ameeleza kuwa jumla ya wafanyabiashara 537 waliojenga mabanda, maduka, ama nyumba zao kwenye maeneo ya hifadhi ya barabara Barabara wanatarajiwa kuondolewa mara moja Mkoani Kigoma hususan katika Manispaa ya Kigoma ujiji, Kasulu na Kibondo.
Akiongea katika kikao hicho Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Kigoma Mhandisi Choma amesema agizo hili linazingatia Sheria ya Barabara Namba. 13 ya mwaka 2007 ambayo inazuia kujenge, au kufanya biashara ya aina yoyote kwenye hifadhi ya barabara.
Kwa sasa wahusika wanaofanya shughuli mbalimbali katika maeneo ya barabara wamekwishajulishwa kwa utaratibu wa barua, ambapo amewataka wenye karakana za magari, pikipiki na bajaji waanze kuondoa vitu vyao kwa hiyari kabla mamla ya TANROARDS haijaanza kutekeleza zoezi la kuwaondo wahusika ikiwemo kuboboa.