Shughuli za kibinadamu pamoja na changamoto za uwepo wa majanga ya Asili zimetajwa kuwa sababu ya kuongezeka kwa kina cha maji katika Ziwa Tanganyika.
Hayo yamebainishwa kupitia mawasilisho ya Mkutano wa Mwaka wa Kamati za kukabiliana na majanga katika mkoa wa Kigoma na mikoa jirani ya nchi ya Burundi uliofanyika katika Ukumbi wa NSSF, Manispaa ya Kigoma Ujiji, mjini hapa.
Imebainishwa kuwa tafiti zilizofanywa zimeonesha athari za majanga ya Asili ikiwemo milipuko ya Volkano katika baadhi ya milima nchini Congo DR, imesababisha lava iliyopoa pamoja na udongo kuingia katika mto Lukuga na kuzuia maji kupita kwa ufanisi ili kuingia katika bahari ya Atlantic.
Aidha kupitia mkutano huo, imebainika kuwa ongezeko la shughuli za kibinadamu pembezoni mwa mto Lukuga, zinasababisha mmomonyoko wa ardhi hivyo mchanga huingia katika mto huo na kutoruhusu maji kupita kwa ufanisi kutoka Ziwani na kuingia baharini.
Baadhi ya athari zilizotajwa kujitokeza kutokana na changamoto ya kuongezeka kwa kina cha maji katika ziwa hilo ni pamoja na Maji kujaa katika maeneo yaliyojengwa miundombinu hususani bandari, makazi, kupotea kwa fukwe, uwepo wa mafuriko kutokana na mito kushindwa kuingiza kungiza Maji Ziwa Tanganyika na kusababisha uharibifu wa makazi pamoja na mashamba.
Katika hatua nyingine wajumbe wa kikao hicho wameafikiana kuushauri uongozi wa serikali za Tanzania, Burundi na Congo DR kuweka mikakati mipya ya udhibiti wa shughuli za kibinadamu zinazosababisha uharibifu wa mazingira katika ziwa hilo na maeneo jirani ikiwemo kuongeza kasi katika usimamizi wa matumizi bora ya ardhi.
Aidha, katika kukabiliana na majanga kikao hicho kimeainisha changamoto zinazokinzana na juhudi za kufikia malengo ya kamati hizo ikiwemo ufinyu wa bajeti, wakazi kukosa elimu ya kukabiliana na majanga, uharibifu wa Mazingira, uhamiaji haramu pamoja na matumizi hafifu ya Teknolojia katika kukabili majanga.
Sambamaba na hayo, wajumbe wa mkutano wamekubaliana kwenda kusimamia uzingatiaji wa mikakati ya pamoja iliyowekwa kwa ajili ya kukabiliana na majanga kwa kuishusha ngazi za chini ili iweze kutekelezwa na wananchi ambao ndio walengwa.
Ongezeko la maji katika ziwa Tanganyika, uhamiaji holelea wa wakazi wa maeneo hayo kwa lengo la kutafuta fursa za kimaisha na usalama, milipuko ya magonjwa pamoja na uharibifu mkubwa wa Mazingira vikiainishwa na mkutano huo kuwa ni sehemu kubwa ya majanga yanayowakabili wakazi katika mkoa wa Kigoma na mikoa jirani ya nchi za Congo DR na Burundi.
Mkutano huo wa wadau hao wa majanga umefadhiliwa na Mashirika yasiyo ya kiserikali ya REDESO na Help Age Tanzania kwa lengo la kuunga mkono kuhamasisha utayari na kuunda mfumo wa pamoja wa tahadhari katika kukabili majanga kwa mikoa hiyo jirani katika nchi hizo.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa