Shirika la Thamini Uhai lafaulu kutoa huduma za dharura za Uzazi Wilayani Uvinza.
Posted on: September 20th, 2017
Moja ya agenda ya Malengo Endelevu ya Milenia 2030 ni kuhakikisha suala la Afya ya uzazi inaimarishwa kwa watu wote na umri wote, kuhakiksha vifo vya mama mjamzito na mtoto mchanga vinapungua chini ya 70% kwa vizazi 10000 duniani; hata hivyo bado changamoto ya huduma za afya za mama na mtoto katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara bado lina changamoto hususan ukosefu wa wataalam wa afya, madawa, miundombinu mibovu ya afya.
Suala la vifo vya kinama wajawazito ni moja ya matatizo makubwa ambayo linatakiwa kupewa kipaumbele na wataalam wa afya, mashirika na asasi mbalimbali. Thamini Uhai ni shirika la kitanzania linalojihusisha zaidi na uhifadhi,uokoaji na uboreshaji wa maisha ya kina mama na watoto wachanga katika mikoa ya Kigoma,Morogoro na Pwani likishirikiana na serikali.Shirika hili linafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na shirika la Vital Strategies lililo na makao makuu huko jijini New York, Marekani.
Katika Mkoa wa Kigoma vifo vya kinama na watoto wachanga kwa muda murefu vimekuwa tatizo hasa kwa maeneo ya vijijini ambapo kinamama wengi hawana utamaduni wa kuhudhuria kliniki, hujifungulia majumbani na kukosekana kwa huduma na miundombinu ya afya ya kinama wajawazito. Shirika la Thamini Uhai Mkoani Kigoma baada ya kufanya utafiti katika upatikanaji wa huduma za rufaa ya mama mjamzito likaja na Mradi wa Afya ambao ni shirikishi kwa jamii ili kupunguza vifo vya kinamama wajawazito na watoto.
Hadi kufika mwaka huu Thamini Uhai likishirikiana na serikali na wadau wengine kujenga uwezo na kuboresha upatikanaji wa huduma timilifu za dharura za uzazi(Comprehensive Emergency Obstetric and Neonatal care;CEmONC) katika vituo vya afya 12 na hospitali 3 katika Mkoa wa Kigoma na huduma za kawaida za dharura za uzazi (Basic Emergency Obstetric and Neonatal Care;BEmONC) katika zahanati 18 katika mkoa huu.
Thamini Uhai imejenga vyumba vya upasuaji ikiwa ni pamoja na kutoa vifaa tiba stahiki, wodi za wazazi, kuboresha mifumo ya maji na umeme kwa kuweka jenereta na umeme wa jua yaani solar na kujenga nyumba za watumishi. Kutolewa kwa mafunzo mahsusi kwa watumishi zaidi ya 100, na kuwatembelea mara kwa mara katika vituo vyao ili kujenga uwezo wao wa kuwahudumia akina mama wajawazito na watoto wachanga ili kuhakikisha utoaji wa huduma za dharura za uzazi unakuwa bora zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Thamini Uhai Dkt. Nguke Mwakatundu anaeleza kuwa mambo yanayosababisha vifo vya kinama ni uchelewashaji kwa maana ya jamii kutambua na kuamua wakati gani mjamzito apelekwe kwenye kituo cha afya, miundombinu ya usafiri kutoka nyumbani hadi kwenye huduma,kucheleweshewa huduma mama mjamzito akiwa katika kituo cha huduma. Hivyo kwa kutambua hayo shirika liliamua kwanza kabla ya kuimarisha miundo mbinu ya afya lielimishe jamii itambuae umuhimu wa mama mjamzito kujifunguli katika vituo vya afya.
Kuanzia mwishoni mwa mwaka 2015 , shirika likishirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma lilianzisha mradi wa majaribio wa uboreshaji wa rufaa za wagonjwa kutoka zahanati 5 kwenda kituo cha afya cha Nguruka.Mradi huu ulifadhiliwa na shirika la Svenska PostkodStiftelsen la nchini Sweden, mradi uliomalizika rasmi mwezi Aprili 2017.
Dkt. Stanford Chamgeni ambaye ni Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Nguruka anataja mafanikio ya mradi wa thamini Uhai akisema wananchi wengi wamehamasika kujifungulia katika vituo vya afya, masuala ya upasuaji yamepungua kutoka watu 40-50 kwa mwezi hadi kinamama 2-3 kwa mwezi. aidha mradi umesaidia kusogeza karibu huduma ya kujifungua kwani hapo awali walifuata huduma hiyo Wilayani Urambo Mkoani Tabora.
Katika kipindi kifupi cha utekelezaji wa mradi huu cha takribani mwaka mmoja na miezi sita, mradi umewezesha kutengenezwa kwa mwongozo wa rufaa kwa eneo la Nguruka, kuongezeka kwa wajawazito wanaojifungulia katika zahanati 5 za mradi na kituo cha afya cha Ngurukakwa 15%,kupungua kwa kina mama wanaojifungulia nyumbani, kuongezeka kwa wajawazito wenye matatizo makubwa ya uzazi (complications) wanaotibiwa katika kituo cha afya cha Nguruka kwa 68% na kupungua kwa uchelewaji wa rufaa kati ya zahanati na kituo cha afya cha Nguruka kwa 41 %.
Juma Nzengula Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyangabho tarafa ya Nguruka anatoa ushuhuda wa mafanikio ya Thamini Uhai kwa kutaja hatua zilizochukuliwa na Thamini Uhai zilikuwa shirikishi kwa ngazi ya serikali ya kijiji hadi kwa wananchi. Wananchi walishirikishwa mipango yote na kuamua, ndiyo maana suala la kuchangia gharama za usafiri wa dharula limepokelewa na wanakijiji vizuri sana na wanalitekeleza bila kujali familia inamjamzito ama la. kupitia Thamini Uhai sasa kila kijiji kimeunda mfuko wa dharula kwaajili ya uchangiaji wa gharama za usafiri, juhudi zimepunguza vifo kwa 50%.
Hivi karibuni Shirika la Thamini Uhai ,limekabidhi pikipiki tatu za magurudumu matatu za kubebea wagonjwa kwa Halmashauri ya wilaya ya Uvinza ili kusaidia rufaa za kina mama wajawazito walio katika dharura za uzazi katika maeneo ya vijijini katika kata ya Nguruka, ili kina mama hao waweze kuwaishwa kwenye kituo cha afya cha Nguruka kwa huduma za juu zaidi.
Dkt. Nguke anaeleza kilichowasukuma kutoa msaada wa pikipiki za mgurudumu matatu. Wakati wa utekelezaji wa mradi huu "jamii kadhaa za eneo la mradi ziliomba kusaidiwa kupewa pikipiki za magurudumu matatu ili ziwasaidie vizuri zaidi kupeleka kina mama wajawazito wenye matatizo makubwa kutoka maeneo ya zahanati yaliyopo vijijini na kuwapeleka kituo cha afya cha Nguruka ili kuwa na usafiri bora zaidi ya boda boda sana sana kwa kina mama wenye hali mbaya sana. Mfadhili wamradi baada ya kusikia mawazo haya alikubali zilizogharimu jumla ya shilingi milioni 24 za kitanzania. Pikipiki zitatumika katika zahanati za Chagu,Ilalanguru na Malagarasi.Thamini Uhai inatumaini jamii husika zitanufaika kutumia pikipiki hizi katika kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga.
Mikakati na harakati mbalimbali za kuhakikisha afya na maisha ya akina mama wajawazito na watoto vinaendelea kuwa salama zaidi katika Wilaya ya Uvinza, hasa maeneo yaliyokuwa hayanahuduma hizi. Katika Wilaya ya Uvinza, Nguruka ndiyo Kijiji kilichokuwa kinaongoza kwa vifo vya kinama wajawazito kabla na baada ya kujifungua.
Dkt. Ignus Kalongola anaeleza kuwa Thamini Uhai iliona kunaumuhimu wa kuanza kutoa elimu kwa jamii ili watakapotambua umuhimu wa suala la mjamzito kujifungulia katika kituo cha afya inakuwa rahisi sana hata kutumia rasilimali zitakazowekwa. Wakati mwingine tatizo la vifo vya kinama limekuwa si ukosefu wa miundominu ya afya bali uelewa wa jamii na mazaoea pamoja na mila duni.
Shirika pia limekuwa likifanya mawasiliano na jamii kuhusiana na afya ya mama na mtoto zikiwamo Kampeni za mawasiliano na jamii. Kuboreka kwa mawasiliano kati ya jamii na wasafirishaji wadogo wadogo kama boda boda wakati wa dharura, kusaidia kuboresha kwa mawasiliano ya simu kati ya jamii na vituo vya kutolea huduma na kati ya ngazi mbalimbali za vituo vya kutolea huduma na kuongezeka kwa utayari wa zahanati na kituo cha afya cha Nguruka katika kutoa huduma za dharura za wamama wajawazito.
Mafanikio ya mradi huu yamevutia wahisani wengine wa Bloomberg Philanthropies na H&B Agerup Foundation kukubali kuanzisha mradi wa rufaa katika Wilaya za Kakonko na Kibondo na mchakato wa uanzishwaji wa mradi katika maeneo hayo unaendelea kwa sasa.
Muhamasishaji jamii katika Kijiji cha Bweru Bi. Hadija Idd Isaa anaelezea namna Thamini Uhai ilivyosaidia kupunguza vifo vya kinamama wajawazito na watoto wachanga, "tunashukuru mradi huu kwani tangu kuanzishwa kwake idadi ya wajazazito kujifungulia nyumbani imepungua kwa kiwango kikubwa. Thamini uhai kwanza ilijikita katika kutoa elimu kwa jamii, kutambua, mazingira hatarishi ya wajawazito, kwa kuwashirikisha wakunga wa jadi familia nyingi sasa zinatamua umuhimu wa mama mjamzito kuhudhuria katika vituo vya afya hata wakati wa miezi ya ujauzito".
anaongeza Bi. Hadijah Thamini Uhai katika kupunguza vifo vya mama mjamzito yametokana na uhusishwaji wa jamii husika moja kwamoja kwa kutoa elimu, uhamasishaji na kuwashirikisha jamii katika kupanga mipango mbalimbali inayohusiana na matatizo yanayopelekea vifo vya kkinamama wajawazito. Anaongeza kuwa Mafanikio mengine yalikuwa kuanzishwa kwa mifuko midogo katika jamii katika vijiji vyote 11 vya maeneo ya mradi, michango ambayo inatolewa kwa mwezi kwa kila familia shilling 500 hadi 1000 kwa ajiliya kusaidia kugharamia usafiri wakati wa rufaa za wajawazito wenye matatizo makubwa ndani ya vijiji.