Katika kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imesema itaendelea kuweka mikakati na kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoa mafunzo ya kukabiliana na Maafa yanayoweza kujitokeza ili kupunguza athari zake kwa wananchi mkoani Kigoma na Tanzania kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. Salum Manyata alipozungumza kwenye semina ya kujenga uelewa juu ya upunguzaji wa madhara ya Maafa katika Jamii iliyofanyika katika Halmashauri ya wilaya ya Kigoma iliyowahusisha wenyeviti wa vijiji, watendaji kata na vijiji pamoja na Maafisa kutoka Halmashauri hiyo na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
Amesema mafunzo hayo yamewalenga viongozi hao kwa kuwa kundi hilo lipo karibu sana na wananchi wanaoguswa moja kwa moja na majanga hivyo ushiriki wao utarahisisha kufikisha maarifa hayo kwa wananchi sambamba na kushusha mipango ya kukabiliana na majanga katika ngazi hizo.
‘‘Kupitia semina hii tumewaelekeza namna bora ya kushughulika na majanga kabla, wakati na muda mfupi baada ya majanga kutokea sambamba na kubaini vihatarishi, vilivyopo katika maeneo yao, namna bora ya kutoa taarifa katika mamalaka za juu pamoja na kutoa elimu kwa jamii’’ amesema Dkt. Manyata.
Amesema miongoni mwa sababu za majanga zilizobainishwa na wananchi kupitia washiriki hao kuwa ni pamoja na baadhi ya wakazi kujenga makazi yao katika maeneo yenye miteremko mikali, ujenzi pembezoni mwa ziwa Tanganyika, uwepo wa upepo mkali, mvua za mawe na mmomonyoko wa udongo.
‘‘Mara baada ya kuwajengea uwezo, washiriki hawa wanapaswa kutengeneza mipango ya pamoja itakayoisaidia kamati elekezi ya wilaya na mkoa kuitekeleza mipango hiyo kwa lengo la kuchukua tahadhari au kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kutokana na majanga kwani kwa sasa tumeshatoka kwenye hatua ya kusubiri kukabiliana na majanga na tupo katika hatua ya kuzuia na kujiandaa’’ amesisitiza Dkt. Manyata.
Aidha Manyata amewashauri wataalam wa serikali wanaosimamia utekelezaji wa miradi ya Mendeleo kuzishirikisha kamati za maafa ngazi za kata kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi hiyo ili ziweze kutoa ushauri na kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza iwapo miradi hiyo itatekelezwa katika maeneo yenye viashiria vya majanga yanayoweza kusababisha maafa.
Upande wake mshiriki wa semina hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Bugamba Kata ya Mwamgongo wilaya ya Kigoma Moshi Ahmad amesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo katika kutambua viashiria na hatua za kuchukua kabla, wakati na muda mfupi baada ya kutokea kwa maafa.
‘’Naishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kushirikiana na mdau wa maendeleo Shirika la kimataifa la uhamiaji (IOM) Mkoa wa Kigoma kwa kufanikisha mafunzo yaliyotupa ujuzi huu kwani majanga yamekuwa yakitokea katika maeneo yetu na tukawa hatujui namna bora ya kuyakabili, lakini kwa sasa tumetambua nafasi na majukumu yetu katika kukabiliana na maafa’’ amesema Bugamba.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa