Baadhi ya Watawa waliohudhuria kwenye Ibada ya Jubilei ya Mhashamu Askofu Joseph P. Mlola Mapadre na Watawa wengine iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Bikira Maria Mshindaji mjini Kigoma.
Mgeni Rasmi, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anna Makinda akitoa neno mara baada ya Ibada ya Jubilei ya Baba Askofu Mlola pamoja na watawa wengine iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria Mshindaji jimboni Kigoma.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye, amesema Serikali haitosita kuwachukulia hatua watu wanaovunja Sheria kwa kuvamia Ardhi inayomilikiwa na Taasisi za kidini mkoani hapa.
Mkuu wa Mkoa ametoa Rai hiyo mara baada ya Ibada ya Maadhimisho ya Jubilei ya Askofu Joseph Mlola, Mapadre na Watawa wengine iliyofanyika Katika Kanisa la Bikira Maria Mshindaji Jimbo la Kigoma, ambapo amemuwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango.
Amesema Serikali kwa kushirikiana na wakuu wa Wilaya mkoani Kigoma wataendelea kushughulikia migogoro ya Ardhi na kuipunguza au kuimaliza kabisa kwani maeneo ya Taasisi za Dini yamepimwa na upatikanaji wake umefuata taratibu zote za kiserikali.
Akitoa neno neno la Shukurani, Mhashamu Askofu Mlola amesema waumini waendelee kuwaombea ili wazidi kuimarika katika utumishi wa Mungu huku akisisitiza kuendelea kuimarika kwa Kanisa Katoliki mkoani Kigoma kufuatia kuongezeka kwa miito ya Kitawa na Mashirika ya kitume pamoja na ujenzi wa makanisa.
Pamoja na huduma zinazotolewa na Kanisa hilo Katika Mkoa wa Kigoma, amesema Kanisa linakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa miundombinu ya Nyumba za Mapadre, Taasisi za Elimu na Afya, pamoja na uvamizi wa Ardhi katika maeneo yanayomilikiwa kihalali na Kanisa Katoliki mkoani hapa.
Mgeni Rasmi katika Jubilei hiyo, Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi kwa Mwaka 2022 na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anna Makinda amewapongeza Askofu Mlola na watawa wengine waliokuwa wakiadhimisha Jubilei hiyo ya Utumishi wa Mungu katika Kanisa.
Aidha amesisitiza wakazi kujitokeza na kutoa ushirikiano ili kufanikisha zoezi la Sensa ya watu na makazi huku akifafanua kuwa, zoezi hilo halitakamilika kwa siku moja hivyo watu watatatakiwa kuendelea kutoa taarifa pale watakapofikiwa na Makarani wa Sensa baada ya siku ya uzinduzi.
‘’Siku ya Sensa ya Watu na Makazi, kila mtu ahesabiwe kwenye kaya au eneo alikolala, Sote tuhakikishe tunahesabiwa ili kuipa nafasi Serikali kupanga na kutekeleza Mipango kuendana na idadi yetu’’ amesema mama Makinda.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa