Baadhi ya miche ya Miti aina ya misindano iikiwa imekauka baada ya kunyunyiziwa dawa ya kukausha magugu na wanaodaiwa kuwa ni wavamizi katika Hifadhi ya Msitu wa Makere Kusini. Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye (wa pili kushoto) akitazama Trekta Mali ya Serikali lililochomwa moto na watu wanaodaiwa kuwa ni wavamizi katika Hifadhi ya Msitu wa Makere Kusini.Baadhi ya vitendea kazi vikiwa vimeungua.
Serikali mkoani Kigoma imeagiza kufanyika kwa Operesheni Maalum ya Siku Ishirini na Moja kuanzia leo Tarehe 20 Septemba 2022, ikiwa na lengo la kuondoa wavamizi wanaofanya shughuli za Kilimo na Ufugaji unaosababisha uharibifu wa mazingira Katika Msitu wa Hifadhi ya Makere Kusini uliopo wilayani Kasulu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Opersheni hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mhe. Thobias Andengenye amesema ni marufuku kwa mtu yeyote kuendelea na shughuli za kibinaadamu katika eneo hilo ili lengo la Serikali kulifanya kuwa Hifadhi liweze kutimia.
‘’Sheria za Uhifadhi wa Mazingira zinakataza kinachoendelea kufanyika katika eneo hili, hivyo nawatangazia watu wote kuwa hairuhusiwi kuendelea na shughuli za kilimo, ufugaji na nyinginezo pia atakayekamatwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake’’ amesema Andengenye.
‘‘Naagiza yeyote atakayepata taarifa hii huku akiwa ndani ya mipaka ya hifadhi aondoke mara moja bila kusubiri kushurutishwa na Askari Maalum wa Doria ambao wataanza kuzunguukia maeneo hayo mara baada ya kutolewa kwa tamko hilo.’’ Amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Aidha amesikitishwa na uharibifu mkubwa wa vitendea kazi pamoja na miche ya Miti iliyokuwa ikiandaliwa kwa ajili ya kupandwa katika eneo hilo la Hifadhi ili kukabiliana na uharibifu mkubwa wa mazingira uliofanywa na wavamizi hao.
Naye Mhifadhi Mkuu wa Mradi wa Shamba la Miti Makere Deograsian Kavishe amesema, watu wanaodhaniwa kuwa na uhusiano na wavamizi hao, walivamia Kambi ya Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania(TFS) iliyopo hifadhini humo na kuharibu vitendea kazi pamoja na miche ya Miti iliyokuwa imeoteshwa katika eneo hilo.
‘’Wavamizi walivamia na kuteketeza mali mbalimbali ikiwemo kuchoma moto Hekta zaidi ya Mia moja za miti iliyopandwa, Trekta, Miche elfu tano ya miti aina ya Misindano, mashine za kusukuma Maji, matoroli pamoja na vifaa vingine vikiwa na Thamani ya Shilingi Milioni mia nne na hamsini.
Mhifadhi huyo amewataka wananchi kuheshimu Sheria za Nchi na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Serikali ili kuepuka uvunjifu wa Amani.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa