NAIBU KATIBU MKUU OFISI YA RAIS MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA XAVIER DAUD AKISALIMIANA NA MKUU WA MKOA WA KIGOMA THOBIAS ANDENGENYE ALIPOWASILI MKOANI HAPA KWA AJILI YA KUFUNGUA KIKAO CHA ROBO YA TATU CHA KAMATI YA KITAIFA YA UKIMWI, VVU NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA MAHALI PA KAZI KATIKA UTUMISHI WA UMMA.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Xavier Daud amesema serikali itaendelea kukabiliana na changamoto zinazohatarisha usalama wa Afya kwa Watumishi wa Umma ili na kuwawezesha kumudu kutoa huduma bora kwa wananchi.
Naibu Katibu Mkuu ametoa wito huo alipozungumza wakati akifungua Kikao cha Robo ya Tatu cha Kamati ya kitaifa ya kudhibiti UKIMWI, VVU na Magonjwa yasiyoambukiza mahali pa kazi katika utumishi wa Umma, kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma na kusisitiza watendaji hao kudumisha usalama wa Afya zao ili waweze kumudu majukumu yao ya kiutendaji kazi Serikali.
‘’Kwa mwaka 2017 nchi ilikuwa na wagonjwa 688901 wenye magonjwa sugu yasiyoambukiza ambapo hadi kufikia mwaka 2022 kulikuwa na wagonjwa 1,456,881 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya Asilimia hamsini, yakihusisha maradhi ya Shinikizo la damu, uzito uliozidi, Afya ya akili pamoja na kisukari’’ amesema Naibu Katibu Mkuu.
Amezitaja tabia na mienendo inayosabababisha ongezeko la magonjwa hayo kuwa ni pamoja na tabia bwete, kutozingatia taratibu za ulaji, matumizi ya vileo na kutokuzingatia ratiba ya ufanyaji mazoezi.
‘’Tumeendelea kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kufanya matibabu badala ya kutumia gharama ndogo kwa ajili ya kujikinga na maradhi hayo, hali inayochangia kupoteza rasilimali fedha pamoja na muda mwingi kwa ajili ya kushughulikia matibabu’’ amesisitiza Daud.
Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa amesema moja wapo ya changamoto kubwa kwa watumishi wa Umma ni suala la Afya ya Akili kutokana na wengi wao kukumbwa na hali ya msongo wa mawazo na kukosa wataalam wa masuala hayo katika Taasisi za Umma kwa ajili ya kuwasaidia kutatua changamoto hiyo.
''Kupitia kikao hiki wajumbe mnapaswa kutoka na maazimio yatakayoisaidia serikali kuona namna bora ya kutatua tatizo la Afya ya akili kwa watumishi wa Umma ili kuwanusuru na maamuzi wanayoweza kuyafanya wakiwa katika hali hiyo yanayoweza kuwaathiri wao wenyewe au wananchi wanaowahudumia'' amesema Rugwa.
Emma Lyimo, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu OR-TAMISEMI ambaye ni mjumbe wa kikao hicho amesema lengo la kikao ni kupata Taarifa za hali ya maambukizi ya UKIMWI, VVU na Magonjwa sugu yasiyoambikuza kutoka ngazi za Mamlaka za Serikali za Mitaa hadi Wizara.
Amesema taarifa zilizowasilishwa zinaonesha kuwa bado kunachangamoto kubwa katika muitikio wa watumishi wa Umma kujitokeza na kupima maradhi ya UKIMWI,HIV na Magonjwa sugu yasiyoambukiza pamoja na kutokuwa tayari kuipokea elimu na kuwa tayari kudhibiti changamoto hizo.
‘’Watumishi wengi wa Umma hujikuta wakikaa ofisini muda mrefu, kula vyakula bila kuzingatia ratiba au makundi ya vyakula pamoja na kushindwa kufanya mazoezi jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa Afya zao’’ amesema.
‘’Watendaji katika Ofisi za Utumishi wahakikishe kunakuwepo na ratiba za watumsihi kushiriki michezo ikiwemo kufanya mazoezi ya viungo, kupima maendeleo ya hali za kiafya pamoja na kupunguza tabia za kushinda kazini badala ya kutumia muda wa ziada kushirki masuala ya kijamii’’ amesisitiza Lyimo.
Upande wake Mhasibu Mkuu wa Mkoa wa Kigoma CPA Johson Gamba amesema Mazingira ya kazi ikiwemo uwepo wa mfululizo wa majukumu yameendelea kuwa changamoto na kisababishi kikubwa kwa wafanyakazi kukumbwa na maradhi sugu yasiyoambukiza.
‘’Nashauri serikali ifanye utafiti na ije na mapendekezo yatakayosaidia kubaini na kutoa miongozo itakayosaidia kubadili mitindo ya maisha ili kuendana na hali halisi ya mazingira ya kazi na kuzikabili changamoto zitokanazo na magonjwa sugu yasiyoambukiza miongoni kwa watendaji wa Serikali’’ ameshauri Gamba.
Mratibu wa UKIMWI, VVU na Magonjwa yasiyoambukiza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Zabibu Mkamba amesema mpaka kufikia mwaka 2024 jumla ya watumishi 30 Wenye maradhi ya VVU na UKIMWI pamoja na 98 wenye magonjwa yasiyoambukiza wametambuliwa kupitia waratibu wa kiafya kutoka mamlaka ya Serikali za Mitaa na tayari wanaendelea kupatiwa huduma maalum za kiserikali.
Aidha kupitia kikao hicho, Mkamba amesema waratibu wa maradhi hayo wamepewa maelekezo ya kuhakikisha wanaendelea kuwatambua watumishi wenye changamoto hizo katika maeneo yao sambamba na kuendelea kutoa elimu na hamasa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa