Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri za Wilaya za Wilaya Mkoani hapa wametakiwa kuongeza kasi ya uchangiaji fedha kwenye mfumo wa M-Mama sambamba na kuwalipa Madereva Jamii wanaoendesha magari yanayotoa huduma hiyo ili kuwezesha zoezi la kuwafikisha wajawazito na watoto katika vituo vya kutolea huduma za Afya kwa wakati.
Akizungumza kwenye kikao cha wadau cha kukabidhi Mfumo wa M-Mama kwa Serikali ya mkoa wa Kigoma, kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa wilaya ya Kigoma Salum Kalli amesema iwapo Halmashauri zitaupokea mfumo huo na kuzingatia miongozo ya uendeshaji wake itasaidia kuendelea kupunguza vifo vya wanawake na watoto ili kudumisha uzazi salama.
Mhe. Kalli amesema watendaji hao kwa kushirikiana na wasimamizi wa mfumo wanapaswa kuimarisha uwajibikaji ili kuufanya mfumo huo kuwa endelevu na kutimza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha changamto ya vifo vya wajawazito, wanawake wanaojifungua pamoja na watoto inamalizika mkoani Kigoma.
Kupitia kikao hicho Mhe. Kalli amewahimiza wakazi mkoani hapa kuzingatia ulaji mlo kamili ili kulinda Afya zao dhidi ya maradhi yanayoweza kuzuilika kupitia ulaji wa chakula bora.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wakazi mkoani hapa kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maradhi mbalimbali ikiwemo kuzingatia kaninu za Afya pamoja na namna bora ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko.
Upande wake mratibu wa Mfumo ngazi ya Mkoa Bernadetha Peter amesema, jumla ya wateja 2,598 wamefanikiwa kusafirishwa ili kuvifikia vituo vya kutolea huduma ya Afya tangu kuanzishwa kwa mfumo huo mkoani Kigoma Aprili 20,2024 huku idadi ya wanawake ikiwa 2,220 na watoto 368.
Amesema mara baada ya mfumo kukabidhiwa serikalini, wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wanapaswa kuhakikisha Idara ya Fedha na Afya katika halmashauri zao zinasimamia uendeshaji wa mfumo kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na seikali ili kufikia malengo yaliyowekwa.
Ameeleza kuwa, Mfadhili Mkuu wa Mradi Kampuni ya Vodafone kwa kushirikiana na wadau wanaotekeleza uendeshaji wa mfumo huo Shirika la Pathfinder International pamoja na Touch Health wanakabidhi rasmi mfumo huo katika mamlaka ya Mkoa hivyo Halmashauri zitapaswa kuendeleza majukumu ambayo wadau hao walikuwa wakiyatekeleza.
Ameyataja mambo ya kuzingatia ili halmashauri ziweze kufanikiwa katika utekelezaji mpango huo kuwa ni pamoja na wafawidhi wa vituo kusimamia rufaa zote za mama na mtoto ili ziwe kwenye mfumo wa M-Mama, kuidhinisha malipo sahihi na kwa wakati kwa madereva Jamii pamoja na waganga wakuu na kamati za Afya wilaya kusimamia na kutoa taarifa kwa wakati.
‘’Nitoe rai kwa Uongozi wa Halmashauri kufanya malipo ya madereva kwa wakati sambamba na kuhakikisha gari za kusafirisha wagonjwa zinakuwa na mafuta ya kutosha ili ziweze kutumika muda wowote inapohitajika kufanyika hivyo’’ amesema Mratibu wa mfumo huo Bernadetha Peter.
Aidha ameyataja mafanikio ya mpango huo tangu ulipoanzishwa mkoani Kigoma kuwa ni pamoja na vituo vyote 291 kutumia Namba 115 wakati wa dharura ya mama na mtoto, uelewa wa jamii na wadau wote kuhusu umuhimu wa mfumo huona kuhakikisha unaimarika sambamba na kuendelea kufanyika kwa mawasiliano ya haraka miongoni mwa watumiaji wa mfumo.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa