Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mhe. Thobias Andengenye na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Batilda Buriani Leo Januari 6, 2023 wamesafiri kwa Treni wakitumia mabehewa Mapya na ya kisasa yaliyonunuliwa na Serikali kwa ajili ya Reli ya kati na Kaskazini, kutoka Tabora hadi Kigoma kwa Lengo la kujionea hali halisi ya usafiri huo na kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR baina ya Mikoa hiyo pamoja na kuendelea kuboresha miundombinu ya Usafirishaji katika reli hiyo.
Mara baada ya kufika Mkoani Kigoma wakuu hao walipata fursa ya kuzungumza na wananchi, viongozi wa Serikali, taasisi binafsi pamoja na wadau mbalimbali wa Maendeleo waliojitokeza kuupokea msafara huo, ambapo kwa pamoja walimpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuidhinisha Fedha kiasi cha Shilingi Trilioni. 6.34 kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa SGR- awamu ya pili kipande cha Tabora-Kigoma chenye urefu wa Kilomita 506.
Upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema wananchi wanapaswa kutumia fursa ya ujenzi wa Miundombinu hiyo ya Reli kwa lengo la kujiimarisha kiuchumi kwa kuwa gharama za usafiri na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali za kibiashara zitashuka na kufika kwa wakati.
Andengenye ameipongeza Serikali kwa kununua mabehewa mapya 22 ya kusafirisha abiria na kuwaasa wananchi kutumia usafiri wa treni kutokana na unafuu wa gharanma za nauli pamoja na maboresho makubwa yanayoendelea kufanywa na Mhe rais katika miundombinu ya reli.
‘‘Nimesafiri kwa kutumia mabehewa haya na nimejionea mwenyewe ni mapya na yana hadhi ya kuitwa ya kisasa hivyo niwasihi mnapoyatumia kusafiri mhakikishe mnayatunza ili yaweze kudumu na kurejesha fedha tulizowekeza’’ amesema Andengenye.
Amesema Rais Dkt. Samia ameendelea kuufungua mkoa wa Kigoma kwa kuboresha usafiri katika njia za Maji, kupanua Uwanja wa ndege, kujenga Barabara pamoja na kuimarisha mahusiano na nchi jirani za Congo na Burundi.
Naye Dkt. Buriani amesema wananchi waendelee kuwapuuza wanaobeza kazi nzuri zinazoendelea kutekelezwa na Mhe. Rais Samia Suluhu kwani zinazidi kuliimarisha Taifa kiuchumi na kulifanya liweze kujitegemea .
‘‘Mikopo inayokopwa na Serikali si chefuchefu bali ni mikopo yenye malengo ambayo kila mmoja wetu anaona matokeo yake, hivyo tunaendelea kumpongeza Mhe Rais kwa kutafuta fedha kwa ajili ya kuliendeleza Taifa’’ amesema Buriani.
Katika Msafara huo, Viongozi hao wameambatana na Wenyeviti wa CCM(M) Tabora na Kigoma, Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Tabora, Katibu Tawala, Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Tabora, Viongozi Taasisi binafsi pamoja na waandishi wa Habari.
Pamoja na Safari hiyo, Kamati za Ulinzi na Usalama Mkoa wa Kigoma na Tabora watakutana Januari 7, 2023 kwa ajili ya kufanya kikao cha Pamoja cha ujirani Mwema.
PICHA MBALIMBALI ZA MATUKIO YALIYOJIRI KATIKA SAFARI HIYO YA KUMPONGEZA MHE. RAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa