Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini (RITA) unatarajia kuzindua mpango wa uhamasishaji wa usajili wa watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano bure ili waweze kupatiwa vyeti vya kuzaliwa.
Hayo yamebainishwa kupitia Semina ya Siku moja iliyofanyika mkoani hapa ikihusisha viongozi waandamizi wa Serikali wakiwemo Katibu Tawala Mkoa, Wakuu wa Wilaya, wataalam kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Kamati ya Usalama Mkoa, Makatibu Tawala wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Viongozi wa Dini pamoja na wazee Maarufu ikilenga kutumia nafasi zao kuhamasisha Jamii kushiriki kwenye zoezi hilo.
Naibu Kabidhi Mkuu wa Serikali RITA, Irene Lesulie amesema kuwa mpango huo unalenga kubaini, kusajili na kutoa vyeti kwa watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano waliozaliwa nchini kufuatia uwepo wa idadi ndogo ya waliosajiliwa na kupewa vyeti ikilinganishwa na idadi halisi ya watoto waliozaliwa.
‘’Kwa mwaka 2022 jumla ya watoto 442,662 walizaliwa mkoani Kigoma ambapo kati yao ni watoto 46,480 walisajiliwa na kupatiwa vyeti ikiwa ni sawa na Asilimia 10 ya watoto waliozaliwa mwaka huo’’ amesema Lesulie.
Amesema zoezi la usajili na utoaji wa vyeti limekuwa likisuasua na kusababisha idadi ya wanaosajiliwa ili kupata vyeti kuwa ndogo hivyo mpango huu umelenga kufanya uhamasishaji ili kuongeza idadi ya watoto watakaosajiliwa na kupata vyeti kwa kuwasogezea karibu huduma kupitia vituo vya kutolea huduma za Afya na Ofisi za watendaji wa kata.
Akizungumza wakati wa akifungua Semina hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Masala amesema mpango huo utatoa fursa kwa Serikali kupata taswira ya hali halisi ya mahitaji ya kundi hilo pamoja na kupanga mipango ya Maendeleo mkoani Kigoma.
Masala amewataka watendaji wa Serikali wanaosimamia utekelezaji wa zoezi hilo kuhakikisha taratibu za upekuzi na utambuzi wa wanaostahili kupatiwa vyeti hivyo zinazingatiwa na kutekelezwa kwa ufanisi.
Pamoja na hilo, Kanali Masala amesema zoezi hilo halina uhusiano wowote na utoaji wa Uraia wa Tanzania na wale wenye uhitaji huo wahakikishe wanazingatia taratibu rasmi zilizowekwa na Serikali.
Upande wake mwakilishi kutoka OR-TAMISEMI Mariam Mkumbwa amewataka watendaji wanaosimamia zoezi hilo kuhakikisha taarifa zote zinazokusanywa zinaingizwa kwenye mfumo ili mara baada ya usajili taarifa za watoto hao ziweze kusomeka kwenye mifumo mingine ya kiserikali.
Mpango wa usajili kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ulianza mwaka 2013 ambapo hadi kufikia Mwaka 2023, jumla ya watoto Milioni 8.6 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa