Wakala wa Nishati Vijijini ulianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 8 ya Mwaka 2005 kwa lengo la kuhamasisha upatikanaji wa Huduma Bora ya Umeme katika maeneo yote ya vijijini huku ukiwa na dhamira ya kutoa huduma ya kisasa ya Usambazaji wa nishati rahisi na salama, kwa ufanisi huku ikiwa rafiki kwa Mazingira.
Dhamira ya Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ni kuhakikisha huduma hiyo muhimu inawafikia watanzania wote Tanzania Bara katika maeneo ya vijijini.
Mkoa wa Kigoma umeendelea kunufaika na huduma za REA, ambapo wilaya zote sita(6) za mkoa zimefikiwa kwa kiwango tofauti, ambapo hadi kufikia Septemba 2022 jumla ya Vitongoji 883 kati ya 1,855 vimekwisha kuunganishwa na miundombinu ya huduma hiyo.
Wakala huo umeendelea kutekeleza miradi ya kupeleka Umeme katika Wilaya za Kasulu, Kigoma vijijini, Buhigwe, Kibondo, Uvinza na Kakonko kupitia awamu mbalimbali kwa kuzingatia hali ya upatikanaji wa Fedha kuendana hali ya bajeti, japo baadhi ya maeneo miradi imekuwa ikichelewa kiutekelezaji kutokana na changamoto za watendaji pamoja na upatikanaji wa vifaa.
Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy anasema kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguuko wa Pili ulianza kutekelezwa Mwezi Aprili 2022 chini ya Mkandarasi Mzawa State Electrical and Technical Service wenye Thamani ya Shilingi Bilioni 47,176,369,574.58 ukilenga kupeleka umeme katika vijiji 89 kwa wilaya sita za mkoa.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika Oktoba 2022, ambapo mpaka sasa mkandarasi yupo kazini na kazi zilizokamilika ni usanifu wa michoro kwa wilaya zote sita, uandaaji wa njia za umeme pamoja na uchimbaji wa mashimo ya nguzo, kazi zinazoendelea katika wilaya za Kasulu, Buhigwe, Kigoma Vijijini na Kakonko.
Mha. Hamisi anasema mradi mwingine unaotekelezwa ni REA Awamu ya Tatu Mzunguuko wa Kwanza wenye Thamani ya Shilingi Bilioni 13,315,362,802.32 unaotekelezwa na Mkandarasi M/S TANESCO kupitia Kampuni Tanzu ya ETDCO, unaendelea huku malengo ikiwa ni kufikisha nishati hiyo muhimu katika vijiji 69 vya Wilaya za Kakonko na Kibondo.
Anasema kupitia mradi huu, vinini 25 kati ya 29 vimeunganishwa na Umeme katika wilaya ya Kakonko huku vijiji 31 kati ya 40 vikiunganishwa kwa wilaya ya Kibondo ambapo hadi kufikia mwezi Disemba 2022 vijiji 13 vilivyosalia kwa wilaya zote mbili vitakua vimeunganishwa na huduma hiyo.
Utekelezaji wa Mradi wa Awamu ya Tatu Mzunguuko wa Kwanza unaotekelezwa na Mkandarasi M/S CCCE Etern ulioidhinishiwa Shilingi Bilioni 38,623,349,313.29 umekamilika huku vijiji 87 vikiwa vimeunganishwa na miundombinu ya Umeme katika wilaya za Kasulu, Uvinza, Buhigwe na Kigoma vijijini.
Mha. Hamisi anasema, licha ya utekelezaji wa kazi hizo za kuunganisha Nishati hiyo muhimu kwa maendeleo ya wanakigoma, maeneo mengi ya vitongoji bado hayajafikiwa kutokana na baadhi kuwa katika hatua za uhakiki, kutofikiwa na awamu za utekelezaji pamoja na utayari wa Bajeti katika kuyalenga maeneo hayo.
Aidha ametaja sababu nyingine zinazosababisha kutofikiwa kwa malengo yanayowekwa katika mikataba kuwa ni kasi ndogo ya wakandarasi katika kutekeleza miradi, changamoto ya upatikanaji wa vifaa kwa wakati pamoja na baadhi ya wananchi kuhujumu miundombinu ya umeme inayoendelea kuwekwa.
Mhandisi Hamisi amezitaja hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa katika kukabiliana na changamoto hizo ikiwemo baadhi ya wakandarasi wanoshindwa kutekeleza miradi yao kwa wakati kupewa onyo au kusitishiwa mikataba yao ya kazi na kupewa wakandarasi wengine. Aidha wamekuwa wakiikabili changamoto ya kupanda kwa bei za vifaa kwa kupitia upya mikataba na kurekebisha bei kuendana na hali ya soko la vifaa.
Katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa miundombinu ya umeme, REA inaendelea kutoa Elimu na Hamasa ya utunzaji miundombinu hiyo kwa maslahi mapana ya watanzania wote huku wakiahidi kupeleka umeme katika vitongoji vyote 972 vya Mkoa wa Kigoma ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo muhimu kutegemea hali ya upatikanaji wa Fedha.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa