Wafanyabiashara ndogondogo mkoani Kigoma wametakiwa kutumia vitambulisho vya kisasa vya wafanyabiashara kwa lengo la kujenga Mazingira rafiki ya kibiashara na kujinufaisha kiuchumi.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye ametoa wito huo alipozungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara kwa mkoa wa Kigoma ambapo jumla ya vitambulisho 1453 vimegawiwa kwa awamu ya kwanza katika Halmashauri nane za mkoa wa Kigoma.
Amesema vitambulisho hivyo vimeunganishwa na mfumo wa NIDA na kimetengenezwa kwa Teknolojia inayomwezesha mtumiaji kufanya miamala ya kifedha na kukitumia kama dhamana.
Kupitia hotuba yake, Andengenye ametoa wito kwa Uongozi wa Halmashauri za Mkoa kuendelea na zoezi la utambuzi na usajili wa wafanyabiashara kwa ajili ya kupata vitambulisho hivyo sambamba na kuhamasisha wafanyabiashara kuendelea kujisaji kupata vitambulisho hivyo kwa wakati.
Andengenye ameishukuru serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuweka mifumo rafiki ya kibiashara kwa wafanyabiashara wadogo, wakati na wale wenye mitaji mikubwa mkoani Kigoma sambamba kuendelea kuimarisha miundombinu wezeshi ili kulifanya kundi hilo kufikia malengo waliyojiwekea na kuimarisha uchumi wa nchi.
Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Bi. Mwajuma Ali amesema mpaka kufikia Desemba 2024 mkoa umefanikiwa kusajili wafanyabiashara ndogondogo 2578 ambapo lengo ni kusajili wafanyabiashara zaidi ya 5500 ifikapo Juni,2025.
Mwajuma ametoa mchanganuo wa ugawaji wa vitambulisho hivyo ambapo Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe imepata vitambulisho 13, Kasulu 355, Kakonko 302, Kibondo 154, Kigoma 94, Uvinza 202, Manispaa ya Kigoma Ujiji 250 pamoja na Hamlashauri yaMji wa Kasulu vitambulisho 83.
Aidha, amewasisitiza wafanyabiashara ndogondogo mkoani Kigoma kuendelea kujisajili ili waweze kuingia kwenye mfumo huo wa kisasa ambapo mpaka kufikia Desemba 12, 2024 jumla ya wafanyabiashara 2578 wamekwisha sajiliwa sambamba na kulipia Ada ya usajili.
Upande wake mnufaika wa vitambulisho hivyo na mfanyabiashara ndogondogo Manispaa ya Kigoma Ujiji John Mbuwa amesema vitambulisho hivyo vimekuwa ni sehemu ya kurasimisha biashara zao.
Amesema utaratibu huo utawapa uhuru wajasiriamali wadogo hususani waliopo katika sekta ya Biashara.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa