Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye leo Novemba 11,2024 amezindua rasmi Kampeni ya kuwaandikisha na kuwarejesha shuleni watoto walio nje ya Mfumo wa Shule ngazi ya ELIMU Msingi wanafunzi waliokatisha masomo mkoani Kigoma kwa sababu mbalimbali ikiwemo vikwazo vya kijamii na kifikra.
Kampeni hiyo inaratibiwa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto katika Mataifa yanayoendelea(UNICEF) imelenga kuondoa vikwazo ambavyo vimekuwa vikichangia watoto kushindwa kufikia malengo yao ya kitaaluma ikiwemo ukosefu wa vifaa vya shule,utoro, Imani za kishirikina, mila potofu, matumizi ya watoto kama nguvu kazi ya familia, hofu kutokana na adhabu shuleni pamoja na migogoro ya kifamilia.
Amesema katika kipindi cha Mwaka 2023/2024 wanafunzi walioandikishwa nje ya Mfumo rasmi mkoani Kigoma ni 12517 ambapo wavulana wakiwa 6515 na wasichana 6002. Aidha watoto waliacha utoro na kurejea shule katika kipindi hicho wakiwa 2352 ambapo wavulana ni 1103 na wasichana 1249.
Amesema kwa mujibu wa takwimu za Mwaka 2024, idadi ya watoto walio nje ya mfumo rasmi wa Elimu ni 7,475 ambapo wavulana ni 4,124 na wasichana 3,351, wakiwa na umri kati ya miaka saba hadi 15. ‘‘Lengo letu ni kuhakikisha kwa mwaka ujao wa 2025 tunaandikisha watoto 5,632na kurejesha wanafunzi 2001’’ amesema Andengenye.
Amesema Kampeni hiyo itakuwa na msukumo mkubwa katika kuhakikisha viongozi katika ngazi za vijiji, kata, ngazi za Halmashauri pamoja na kamati za shule ili kuhamasisha na kufuatilia urejeshwaji wa watoto shuleni kwa wale waliocha sambamba na kuwaandikisha shule watoto wote waliofikia umri stahili.
Amesisitiza kuwa, kupitia Kampeni hiyo, Halmashauri za wilaya kupitia kwa wakurugenzi na viongozi mbalimbali zitasimamia ili kuhakikisha uandikishwaji na urejeshwaji wa wanafunzi mashuleni unafanyika sambamba na kudhibiti vichochezi vya watoto kuacha shule ikiwemo ndoa za utotoni, ajira za watoto pamoja na vizuizi vinginevyo vya kijamii.
Sambamba na hayo, mkuu huyo wa mkoa amewahimiza wakazi kushirikiana na viongozi na wasimamizi wa masuala ya kitaaluma ili kudhibiti utoro, kutoa msaada wa kisaikolojia kwa watoto wanaosoma pale wanapokutana na changamoto za kimaisha, kuhimiza nidhamu chanya sambamba na Halmashauri kushirikiana na wadau katika kutoa misaada kwa watoto wanaotoka kwenye kaya zenye uhitaji mkubwa kupitia mpango wa TASAF.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa