Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye amezindua Kampeni ya Matumizi ya Nishati Safi ya Umeme kwa ajili ya kupikia kwa Mkoa wa Kigoma kupitia Programu ya Pamoja ya Kigoma(UN-Kigoma Joint Program) na kusisitiza kuwa Kampeni hiyo itapunguza changamoto za kiafya kwa wakazi na zile za kimazingira zinazoukumba mkoa wa Kigoma kutokana na matumizi ya kuni.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampeni hiyo uliofanyika katika Hoteli ya Lake Tanganyika Mjini Kigoma, Mhe. Andengenye amesema upatikanaji na Matumizi ya Nishati safi unagusa nyanja mbalimbali katika maisha ya wakazi, uendelevu wa viumbe hai sambamba na utunzaji wa Mazingira kwa ujumla.
Andengenye amesema uzinduzi wa Kampeni hiyo ya kupika kwa kutumia umeme ni sehemu ya mabadiliko yanayoendana na kuunganishwa kwa mkoa katika Umeme wa Gridi ya Taifa na kuipa fursa jamii mkoani Kigoma kunufaika kikamilifu na upatikanaji na matumizi ya nishati safi.
Katika hatua nyingine Mhe. Andengenye amefurahishwa na uwepo wa shule za sekondari 17 mkoani humo zinazotumia nishati safi ya Mkaa mbadala kwa ajili ya kupikia na kuachana na matumizi ya kuni na Mkaa.
Upande wake Mwakilishi kutoka TANESCO Makao Makuu, Mha. Samwel Luckas amesema lengo la serikali ni kuhakikisha watanzania wanahamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema mpango huo umelenga kuwawezesha wapishi kuandaa chakula salama, kisafi na kwa gharama nafuu za upishi na kuziwezesha familia kuishi maisha salama kiafya sambamba na kupata nafuu ya kiuchumi.
"TANESCO itaendelea kusogeza karibu huduma za umeme kupitia usambazaji wa huduma hiyo ili kila mwananchi aweze kushiriki kwenye mpango huo" amesema Mha. Luckas.
Naye Mwakilishi kutoka TIB Development Bank Andrew Mwampaghale amesema taasisi yao itaendelea kuhakikisha majiko ya Nishati safi yanapatikana kwa njia ya ruzuku ili kuwapa wananchi unafuu.
"TID kwa kushirikiana na UNIDO tunaendelea kutafuta ufadhili utakaotuwezesha kupata majiko ya Umeme ambayo utafiti unaonesha hayana gharama kubwa kimatumizi na ni salama ukilinganisha na matumizi ya kuni au mkaa" amefanua Mwampaghale.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa