Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amewataka wakazi mkoani hapa kujenga tabia ya kuchukua tahadhari dhidi ya maradhi mbalimbali kwa kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalam wa Afya ili kujikinga na kuepukana magonjwa yanayozuilika.
Wito huo umetolewa na Mkuu huyo wa mkoa alipozungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Kambi ya Matibabu ya Madaktari bingwa wa Dkt. Samia kwa ajili ya kutoa huduma kwa ngazi ya Halmashauri, uliofanyika katika Hospitali ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na kuitaka jamii kuzingangatia usafi wa watu binafsi na Mazingira yao ili kujiepusha na kupunguza athari za Magonjwa.
Amesema pamoja na Serikali kuendelea kufanya kazi kubwa ya kusogeza huduma za kiafya kwa wananchi, kila kila mmoja anapaswa kuchukua hatua ya kujikinga dhidi ya maradhi hayo jambo litakalopuguza idadi ya wagonjwa na athari zake katika jamii.
Aidha mkuu huyo wa mkoa amewakumbusha wakazi kuzingatia ulaji wa mlo kamili ili kupunguza kiwango cha udumavu na utapiamlo kwa watoto kutokana na mkoa kuzalisha chakula cha kutosha.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Kigoma Kaimu Katibu Tawala Mkoa Elisante Mbwilo amewataka wananchi waliojitokeza kupata huduma kupitia madaktari hao kuwa mabalozi kwa kuwafikishia taarifa wahitaji wengine wa huduma hizo waliopo katika maeneo yao.
‘‘Hakikisheni mnawafikishia wengine taarifa kuhusu uwepo wa huduma hii ili waweze kufahamu na kujitokeza kupata matibabu kwa urahisi na ukaribu’’ amesisitiza Mbwilo.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Cephlen Budodi amesema mpaka kufikia Mei 10, 2024 jumla ya mikoa 17 imefikiwa huku zoezi hilo likiwa ni endelevu lililenga kuzifikia Halmashauri zote 184 za Tanzania bara.
Budodi ametoa wito kwa wananchi kufika katika hospitali za wilaya ili kukutana na wataaalam hao ikiwa ni fursa muhimu na adhimu ya kupata huduma hizo katika maeneo yao ya karibu.
Upande Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Lebba amesema jumla ya madaktari bingwa 40 wamepokelewa mkoani humo kwa ajili ya kutoa huduma bobezi za kitabibu katika Hospitali za wilaya zilizopo kwenye Halmashauri nane za Mkoa wa Kigoma.
Amezitaja huduma zitakazotolewa kuwa ni pamoja na matibabu kwa magonjwa ya kina mama na watoto, upasuaji wa aina mbalimbali, magonjwa ya ndani sambamba na utoaji huduma ya kibingwa kwa upande wa usingizi na ganzi.
Dkt. Lebba amefafanua kuwa huduma kutoka kambi hiyo ya madaktari bingwa kimkoa, zimeanza kutolewa Juni 10 hadi 14,2024 na kuwataka wagonjwa kujitokeza ili kutumia fursa hiyo, ikiwa ni muendelezo wa kusogeza huduma hizo kwa wakazi sambamba na kuwaongezea ujuzi madaktari wa ndani wa mkoa.
Jumanne Selemani ambaye ni Mkazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji ameishukuru serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma hiyo katika maeneo ya jirani na kuwapunguzia gharama na muda mrefu wa kufuata huduma hizo nje ya Mkoa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa