Raia wa Kigeni pamoja wakazi wenyeji Mkoani Kigoma wametakiwa kuepuka kufanya udanganyifu ili kupata uhalali wa kupatiwa vitambulisho vya Taifa.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye ametoa Rai hiyo alipozindua zoezi la ugawaji wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ambapo Jumla ya Kadi 77281 zimekamilika na kuanza kukabidhiwa kwa walengwa katika Wilaya ya Kigoma.
Amesema baadhi ya wakazi wasio na sifa pamoja na Raia wa kigeni wamekuwa kikwazo kikubwa katika kuhakikisha zoezi la ukusanyaji taarifa kwa ajili ya kuandaa vitambulisho vya Taifa linafanyika kwa wakati.
Andengenye amefafanua kuwa, kutokana na mkoa kupakana na nchi jirani, kumekuwepo na muingiliano mkubwa wa raia kutoka nchi hizo, ambapo ameahidi Serikali mkoani Kigoma kuendelea kufanyia kazi changamoto hiyo ili wenye zifa waweze kupata vitambulisho kwa wakati.
‘‘Changamoto ya utoaji wa Kadi za Vitambulisho vya Taifa ni endelevu kutokana na ongezeko la wageni pamoja na idadi ya wenye sifa kila siku, hivyo niwasisitize kuendelea kutoa taarifa za kweli na uhakika huku tukiisaidia Serikali kuwabaini wasio na Sifa ili kurahisisha utekelezaji wa zoezi hili’’ amesisitiza.
Aidha Andengenye amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya hususani katika Mkoa wa Kigoma kwa kuendelea kutoa Fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha Miundombinu ya Uchukuzi, usafirishaji pamoja na kuimarisha Sekta za Elimu, Afya na Maji.
Akiwasilisha Taarifa ya utendaji kazi, Afisa Usajili Ofisi ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa Mkoa wa Kigoma Odoyo Godwin amesema mpaka kufikia April 12, 2023 wamefanikiwa kusajili walengwa 967,013 huku waliopata Namba ya utambulisho hadi kufikia tarehe hiyo ikiwa ni walengwa 585,536 na waliopata vitambulisho ikiwa 273,460.
Amefafanua kuwa, kwa wilaya ya Kigoma inayojumuisha Halmashauri ya Kigoma Vijijini pamoja na Manispaa ya Kigoma/Ujiji, jumla ya vitambulisho 77,281 vimekamilika na vinaendelea kugawiwa kwa walengwa.
Amezitaja changamoto zinazochangia kuzorotesha ufanisi na uharaka katika upatikanaji wa vitambulisho hivyo kuwa ni baadhi ya wananchi kujiandikisha zaidi ya mara moja, kutopatikana kwa Namba za Simu zilizotumika wakati wa usajili wa awali pamoja na uwepo wa kundi kubwa la walowezi, wakimbizi pamoja na wageni wakazi.
‘‘Nitoe Rai kwa wanchi wote wanaostahili kupata vitambulisho kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi ili kuepuka usumbufu wa kupata kitambulisho kwa wakati pamoja na kuepuka usumbufu inapotokea taarifa zao kutofautiana pale zinapohitajika kwa ajili ya kufanikisha masuala mbalimbali ya kiserikali’’ amesisitiza Godwin.
Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji waliojitokeza katika hafla hiyo wameipongeza Serikali kwa kufanikisha upatikanaji wa vitambulisho hivyo, huku wakisisitiza watendaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa kuendelea kutoa Elimu kwa wananchi ili kupunguza dosari zinazosababisha walengwa kusubiri kupata vitambulisho hivyo kwa muda mrefu.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa