Pikipiki nane aina ya Boxer zilizotolewa na Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Maendeleo na Ushirika kwa Mkoa wa Kigoma zikiwa tayari kugawiwa kwa Maafisa Ugani wa Halmashauri za Mkoa wa Kigoma leo Tarehe 26, Agosti 2022.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye akijiandaa kuendesha mojawapo ya Pikipiki zilizotolewa kwa maafisa Ushirika Mkoani hapa mara baada ya kuzindua zoezi la makabidhiano ya vitendea kazi hivyo. zoezi hilo limefanyika katika viunga vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
Maafisa Ushirika Mkoani Kigoma wametakiwa kusimamia vyama vya Ushirika kwa nguvu mpya huku wakiyapa kipaumbele makundi Maalum ya kijamii ili yaweze kujikwamua na kujiendeleza kiuchumi.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Ukoaji Thobias Andengenye, wakati wa hafla fupi ya kukabidhi Pikipiki nane zilizotolewa na Serikali kwa Maafisa Ushirika wa wilaya ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema, vyama vya ushirika vijumuishe na kuzingatia makundi ya watu wenye mahitaji Maalum, Bodaboda, Wanawake, wazee, mamalishe na makundi mengine yanayohitaji kupewa kipaumbele ili nao waweze kunufaika na Rasilimali za Serikali.
Amesema pamoja na watendaji hao wa Serikali kuhudumia Jamii kwa ujumla, wanatakiwa kuyatazama makundi hayo, kuyashirikisha na kuyawezesha kikamilifu ili kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotolewa na kusimamiwa na Serikali.
Aidha, amewaasa kutumia vitendea kazi hivyo kwa kuzingatia malengo yaliyokusudiwa na Serikali, na kuepuka matumizi ambayo ni kinyume na malengo jambo ambalo ni ukiukwaji wa maadili ya Utumishi wa Umma.
Pia, ametoa Rai kwa Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia matumizi bora ya vitendea kazi hivyo pamoja na kuwezesha mafuta na ukarabati ili watendaji wasikwame katika utekelezaji wa majukumu yaliyokusudiwa.
Kwa upande wao baadhi ya Maafisa Ushirika, wameishukuru Serikali kwa kuwapatia usafiri hali itakayorahisha kuwatembelea wadau kwa urahisi tofauti na hapo awali, kutokana na baadhi ya maeneo wanayosimamia kiutekelezaji kuwa na tofauti kubwa ya umbali.
Pikipiki hizo aina ya Boxer, zimetolewa na Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Maendeleo na Ushirika kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi kwa Maafisa hao katika majukumu ya usimamizi wa vyama vya ushirika, ukaguzi, utatuzi wa migogoro, usimamizi wa masoko, uhamasishaji na utoaji wa mafunzo endelevu kwa wanachama, viongozi na watendaji wa vyama vya Ushirika.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa