Washabiki na wadau wa Soka mkoani Kigoma wametakiwa kuzidi kuiunga mkono Timu ya Mashujaa FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara (NBC Premier League) Msimu wa 2023/2024 ili iendelee kuwaletea Burudani wanakigoma sambamba na kutangaza fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo mkoani hapa.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye alipozungumza kwenye hafla fupi ya chakula cha usiku aliyoiandaa Mei 23, 2024 kwa lengo la kuwakutanisha pamoja wachezaji, viongozi pamoja na wadau wa Soka mkoani humo, ambapo amesisitiza kuwa pamoja na kutoa burudani kwa washabiki wa mchezo huo, Timu hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kutangaza vivutio vya utalii na uwekezaji vilivyopo mkoani Kigoma.
Aidha katika kuhakikisha timu hiyo inasalia Ligi Kuu msimu wa 2024/2025, mkuu huyo wa mkoa amewaalika washabiki wa mchezo huo ndani na nje ya Mkoa kujitokeza kwa wingi kwa lengo la kuwapa ari wachezaji ili iweze kuibuka na ushindi katika mechi zake mbili zilizosalia ambapo itakabiliana na Timu ya Mtibwa Sugar pamoja na Dodoma Jiji katika Dimba lake la nyumbani la Lake Tanganyika Stadium.
Upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Mkoa wa Kigoma (KFA) Alhaji Ahmed Mgoji amewakumbusha wachezaji wa Timu hiyo kufanya maandalizi ya kutosha ili kuwakabili wapinzani wao na kushinda michezo iliyobaki ili kujiweka katika nafasi nzuri itakayowawezesha kuendelea kushiriki ligi kuu msimu wa 2024/2025.
‘’Michezo miwili iliyobaki tunacheza na timu zinazohitaji matokeo kama ilivyo timu yetu ya Mashujaa, hivyo tunapaswa kupeana mikakati na makujumu ya pamoja ambayo tunapaswa kuyatekeleza ili kuhakikisha timu yetu inashinda na kubaki ligi kuu ya Tanzania bara na kuendelea kuwaletea burudani washabiki wa mchezo huo.
Mwenyekiti wa Mashujaa FC Meja Abdul Tika amesema anaimani na kikosi chake kutokana na ubora wa wachezaji walionao sambamba na timu hiyo kuendelea kuimarika kila siku.
‘’ ligi ya Mwaka huu imekuwa ngumu kutokana na timu zote kutafuta nafasi muhimu ikiwemo nafasi ya pili pamoja na alama chache ambazo timu zimekuwa zikipishana hali inayoendelea kuifanya ligi kuwa ngumu hususani katika hatua za michezo ya mwisho ya ligi.
Naye Nahodha wa Kikosi hicho Maarufu kwa Jina la Mapigo na Mwendo Patrick Munthar amesema kutokana na nafasi waliyopo katika Ligi hiyo, jambo lililopo mbele yao ni kufanya bidi na kushinda michezo hiyo.
‘’Nikuahidi mheshimiwa Mkuu wa Mkoa tutashinda michezo iliyosalia, pia wachezaji wote wameona ni kwa kiasi gani unaguswa na kuwa karibu na Timu hii’’ alisisitiza Munthar
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa