Jamii imetakiwa kujenga utamaduni wa kufanya usafi na kutunza Mazingira katika maeneo wanayoishi ili kudumisha Afya na Mazingira bora ya kuishi.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye alipozungumza mara baada ya kuongoza zoezi la usafi ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani lililofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni Leo Juni 2024.
Amesema suala la uharibifu wa Mazingira limezidi kushika kasi mkoani hapa kutokana na baadhi wakazi kutotilia maanani umuhimu wa kutekeleza maelekezo ya serikali yanayohusu uhifadhi ikiwemo kutunza vyanzo vya maji, kutokata misitu ovyo pamoja na kufanya ufugaji na kilimo cha kisasa.
‘’Tuitumie siku hii kwa lengo la kukumbushana katika kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu zinazoweza kuathiri vyanzo vya Maji, kupanda miti, kulinda maeneo yetu ya hifadhi za mazingira pamoja na kujifunza namna bora ya kuhifadhi au kutokomeza taka katika maeneo tunayoishi’’ amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
Upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Lebba amesema suala la usafi ni msingi wa kupunguza uwezekano wa milipuko ya maradhi mbalimbali na litasaidia katika kulinda Afya zetu.
Aidha amefafanua kuwa kampeni ya kuhimiza usafi kimkoa hususani ujenzi wa vyoo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa ambapo mpaka kufikia mwaka 2024 uwepo wa vyoo kwenye kaya mkoani hapa umefikia asilimia 90.
Lengo la Maadhimisho haya ni kuhamasisha umuhimu wa kulinda na kuhifadhi Mazingira pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali za Mazingira ili kuleta maendeleo endelevu duniani.
Ifahamike kuwa tarehe 5 Juni kila mwaka Tanzania huungana na Jumuia kimataifa kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani ikiwa ni moja wapo ya Maazimio ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira na Maendeleo uliofanyika jijini Stockholm nchini Sweden mwaka 1972.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa