Zaidi ya wakulima 10,000 mkoani Kigoma wamepata mafunzo ya Kilimo Tija ili kuwawezesha kufanya Kilimo cha kisasa kwa lengo la kudhibiti uharibifu mkubwa wa Mazingira pamoja na kupata mazao ya kutosha kwa kutumia eneo dogo.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyowasilishwa kwenye kikao cha tatu cha Kamati Tendaji ya usimamizi wa Mradi wa Kilimo Tija Kigoma (KiTiKi) kilichofanyika katika Hoteli ya Bwami Dubai Mjini Kasulu Leo Mei 22,2024.
Akizungumza mara baada ya kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema Mradi wa KiTiKi unaosimamiwa na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) na kufadhiliwa na Shirika la Ushirikiano la Korea (KOICA) umelenga kuhakikisha wakimbizi wanaendelea kupata chakula kinachozalishwa nchini na kuwanufaisha wakulima wa ndani kupitia kilimo cha Maharage na Alizeti.
Amesema sambamba na kufanikisha kilimo cha mazao, Shirika hilo linatekeleza jukumu la kuwaunganisha wakulima wadogo na Taasisi za kifedha, kuwajengea uwezo ili waweze kuzalisha kwa tija, kuwaunganisha na masoko pamoja na kufanya kilimo cha kisasa na chenye udhibiti wa athari za kimazingira ikiwemo kuachana na kilimo cha kuhamahama.
Ameendelea kueleza kuwa, Kupitia mafunzo yanayotolewa na Programu hiyo, wakulima wanajengewa uwezo katika utunzaji bora wa mazao baada ya kuvuna, kuviimarisha vikundi vya kifedha vilivyoibuliwa miongoni mwao pamoja na kuanzisha vituo vya ukusanyaji wa mazao na uuzaji ili kudhubiti wimbi la udalali linalochangia kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya wakulima.
‘’Kupitia vyama vya Msingi na AMCOS, Wakulima wataweza kuunganishwa na wanunuzi ili kupanga bei ya pamoja yenye tija kwa pande zote katika kuimarisha uchumi wa wakulima wadogo wadogo mkoani Kigoma’’amefafanua Andengenye.
Amesema mradi wa KiTiKi ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa mkoani Kigoma chini ya Programu ya Pamoja ya Kigoma (UN Kigoma Joint Program) kwa sababu ni mojawapo ya eneo yenye jamii liyoathirika kwa kiasi kikubwa na ujio wa wakimbizi kutoka nchini Congo DR na Burundi na kusababisha wakazi wenyeji kupoteza maeneo yao ya asili huku mengine yakiathiriwa kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa mazingira.
‘’ Programu hizi zinaendelea kutekelezwa mkoani hapa ili kuleta unafuu wa kimasiha kwa wakazi wenyeji ambao kwa ukarimu wao wameendelea kujitolea na kupoteza maeneo yao na rasilimali zao kwa ajili ya kuwatunza wenzao ambao wamekimbia nchi zao kutokana na ukosefu wa Amani’’amesisitiza Andengenye.
Upande wake Ihanjam Cha ambaye ni Afisa Mradi wa KiTiKi, amesema malengo ya mradi huo ni kusaidia upatikanaji wa chakula kwa wakimbizi pamoja na kuboresha mahusiano baina ya jamii ya wakimbizi na ile inayozunguuka kambi ambazo ni makazi ya wakimbizi hao.
Aidha amelitaja jukumu lingine la Taasisi hiyo isiyo ya kiserikali kuwa ni kuboresha maisha ya wakulima wadogo wadogo katika wilaya za Kasulu, Kibondo na Kakonko ambazo kwa namna moja au nyingine zimeathirika kwa kiasi kikubwa na uwepo wa jamii ya wakimbizi.
Naye Ali Mwembesazi ambaye ni Makamu Mkuu wa Ofisi ya WFP Kasulu amesema kupitia taasisi ya KiTiKi kwa Msimu wa 2023/2024 imefanikiwa kununua Tani 100 za maharage kutoka kwa wakulima mkoani Kigoma na kuyasambaza katika Kambi ya wakimbizi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo kuendana na malengo ya mradi.
Ameyataja mafaniikio mengine kuwa ni pamoja na kuwafikia wakulima 10,000 na kuwapatia mafunzo ya kilimo bora, uhifadhi wa chakula pamoja na kugeuza shughuli ya kilimo kuwa ajira yenye tita.
‘’malengo yetu kwa mwaka 2024/2025 ni kuhakikisha tunawaunganisha wakulima na Taasisi za kifedha, kutoa mafunzo ya kilimo bora kwa wakulima wapya 10,000 kwa wilaya za Kasulu, Kibondo na Kakonko, ikiwa ni utekelezaji katika mwaka wa pili’’ amesisitiza.
Kupitia kikao chetu tumebaini kuwa changamoto kubwa ni upatikanaji wa mbegu ambapo kwa pamoja tumekubaliana kuandaa programu maalum kwa baadhi ya wakulima ambao ndio watakuwa wazalishaji kisha tukishathibitisha ubora wake tutazisambaza kwa wakulima.
‘’Aidha changamoto nyingine iliyojadiliwa ni pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa hali inayosababisha kupunguza uzalishaji, suala ambalo tumekubaliana na maafisa ugani kushirikiana na wataalam wa hali ya hewa ili kutambua msimu stahili wa kilimo kuendana na mazao husika jambo litakaloepusha hasara kwa wakulima’’ amefafanua Ali.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa