Wakazi wa Mkoa wa Kigoma wametakiwa kutoharibu vyanzo vya Maji kwa kisingizio cha utekelezaji wa shughuli za kiuchumi pamoja na uendelezaji wa makazi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye baada ya kukagua Mradi wa Maji katika kijiji cha Nyakayenzi kilichopo wilayani Kibondo mkoani hapa.
‘’Nasisitiza Sheria ya Utunzaji wa Mazingira pamoja na vyanzo vya Maji ifuatwe ikiwa ni sambamba na uwekaji Alama za mipaka ya hifadhi kwa maeneo hayo na watakaokiuka wachukuliwe hatua mara moja’’
‘‘Tukiendelea kukaa kimya na kutochukua hatua, siku za usoni tutakabiliana na changamoto kubwa ya uhaba wa huduma ya Maji katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wetu'' Amesisitiza Andengenye.
Amesema maeneo mengi ya Mkoa Misitu inaendelea kukatwa ovyo, kumekuwepo na ulishaji holela wa mifugo, uendeshaji wa shughuli za kilimo katika vyanzo vya Maji, pamoja na uvamizi wa maeneo tengefu ya Hifadhi.
Mkuu huyo wa Mkoa, ameishauri Jamii kujenga utamaduni wa kupanda miti rafiki kwa Mazingira hususani katika maeneo ya vyanzo vya Maji ili kujinusuru na uwezekano wa kukabiliana na janga la uhaba wa huduma ya maji katika maeneo mbalimbali mkoani hapa.
Aidha, amewataka wenye jukumu la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira kuongeza nguvu katika utendaji kazi wao kutokana na kuongezeka kwa matukio ya uvamizi na uharibifu wa vyanzo vya maji bila kuchukuliwa kwa hatua madhubuti katika kudhibiti hali hiyo.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa