Wakazi mkoani Kigoma wametakiwa kujenga tabia ya kutunza maeneo ya vyanzo vya Maji ikiwemo kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu pamoja na kupanda miti rafiki kwa mazingira ili kutoviathiri vyanzo hivyo na kuvifanya vidumu na kutoa huduma kwa muda mrefu.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye alipozungumza na wakazi wa wilaya ya Bihigwe alipokagua utekelezaji wa mradi wa Maji Mnanila-Nyakimwe na kusisitiza wakurugenzi wa Halmashauri kushirikiana na mamlaka za kimazingira katika vijiji na mitaa katika kusimamia ulinzi wa vyanzo hivyo.
Amesema kumekuwa na changamoto katika maeneo meng ya mkoa kutokana na baadhi ya wananchi wasio waadilifu kupotosha wenzao kwa kuwahamasisha kutochangia huduma ya maji wakitoa sababu kuwa huduma hiyo ni ya bure ‘’ hii sio sahihi kwani kuna uhitaji mkubwa wa fedha kwa ajili ya gharama za ukarabati wa miundombinu na kuifanya kuwa endelevu’’ amesema Andengenye.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Buhigwe Mha. Golden Katoto amesema mradi wa maji Mnanila-Nyakimwe unatekelezwa kwa Thamani ya Shilingi Bil. 9.7 ambapo utakapokamilika utahudumia wakazi 66,045 katika vijiji vya Bweranka, Kibande, Kitambuka, Nyakimwe, Mkatanga, Kibwigwa, Mnanila na Msagara wilayani humo.
Amesema hatua ya utekelezaji iliyofikiwa ni pamoja na ulazaji wa mabomba, ujenzi wa vituo kumi vya kuchotea maji, majengo ya mitambo, chemba 40 za kuondoa upepo, pamoja na ununuzi wa viungo vingine kwa ajili ya kuunganisha mfumo wa mabomba.
Sambamba na utekelezaji wa kazi hizo, Mhandisi Katoto amesema kazi zinazotarajiwa kuendelea kufanyika ni ujenzi wa matanki mawili ya kuhifadhia maji ambapo kila moja litakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita 1,000,000.
Ameyataja matarajio ya RUWASA mara baada ya kukamilika kwa mradi huo ni pamoja na kuongeza huduma za upatikanaji wa maji kutoka Asilimia 72.2 hadi kufikia 90.2 ambapo mahitaji halisi ya maji katika vijiji hivyo ni lita1,660,125 huku ukitarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 11, 2024.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa