Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Kilimo kwa kuendelea kufanya mageuzi makubwa kwenya Sekta ya Kilimo kwa lengo la kuwawezesha wakulima kufanya kilimo biashara chenye Tija.
Mhe. Andengenye ametoa kauli hiyo alipozungumza kwenye hafla ya kukabidhi vitendea kazi kwa maafisa Ugani Kilimo mkoa wa Kigoma na kusisitiza nyenzo hizo kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na Serikali.
Amesema sekta hiyo ni muhimu kwa ustawi wa Jamii mkoani Kigoma kutokana na zaidi ya Asimilia sabini ya wakazi kutegemea shughuli za kilimo kama chanzo chao kikuu cha uchumi kwa ajili ya kuendesha maisha yao ya kila siku.
‘’Pamoja na Mchango mkubwa wa sekta hiyo katika mkoa wa Kigoma bado wakazi wanafanya kilimo cha kujikimu hivyo dhamira ya serikali ni kufanya mageuzi makubwa kutoka aina hiyo ya Kilimo na kuingia katika mfumo wa kilimo biashara’’ amesema Andengenye.
Kupitia hafla hiyo, mkuu huyo wa Mkoa amegawa magari mawili(2)yaliyotolewa na Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kuratibu shughuli za kilimo ngazi ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe pamoja na mavazi 179 kwa ajili ya Maafisa Ugani Kilimo ngazi ya Mkoa na Halmashauri.
Aidha Mhe. Andengenye amezikumbusha halmashauri kutekeleza maagizo ya Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe ikiwemo halmashauri ya Kigoma Ujijiku kutenga eneo ili wizara hiyo iweze kutekeleza mradi wa ujenzi wa Kituo cha kuratibu shughuli za umwagiliaji nchini.
Sambamba na agizo hilo, Andengenye ameitaka halmashauri ya wilaya ya Kibondo kutekeleza agizo la kutenga eneo ili serikali iweze kutekeleza mradi wa ujenzi wa soko la kisasa la zao la muhogo huku halmashauri ya Buhigwe ikitakiwa kuandaa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata zao la Tangawizi.
Aidha Mhe Andengenye amezielekeza halmashauri zote za mkoa kutenga maeneo ya ujenzi wa masoko ya kimkakati kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kuyafikia masoko hayo na kufanya biashara za mazao yao mazao ya kilimo kwa faida.
Katika hatua nyingine Mhe. Andengenye amekabidhi fedha Taslim kiasi cha Shilingi Mil. 1 kwa niaba ya Waziri wa Kilimo kwa Afisa Ugani Kilimo Manispaa ya Kigoma Ujiji Bi. Sarah Micheal kufuatia waziri huyo kufurahishwa na usimamizi mzuri wa shughuli za kilimo alioufanya mtendaji huyo katika bonde la mto Luiche mkoani hapa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa