Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii Mkoani Kigoma wameishukuru serikali kwa kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa Sekta ya Afya ili kuweka mazingira rafiki yanayowezesha michango ya wadau hao kuigusa jamii kwa kurahisisha utoaji na upatikanaji wa Huduma.
Wakizungumza mara baada ya kukabidhiwa baiskeli ikiwa ni ufadhili kutoka Shirika lisilo la kiserikali Catholic Relief Services (CRS) kwa ajili ya kurahisisha utuatiliaji na utoaji wa huduma, baadhi ya wanufaika wa nyenzo hizo za usafiri wamesema kupatikana kwa vitendea kazi hivyo kutasaidia kuifikia namba kubwa ya wateja wao na kwa wakati sahihi.
Honorina Sunzu ambaye ni muhudumu wa Afya ngazi ya Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma anasema awali walikuwa wakitumia muda mrefu kuwafikia walengwa jambo lililosababisha baadhi yao kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
‘’Nyenzo hizi zimeamsha ari katika utendaji kazi wetu, hivyo tunaishikuru serikali kwa kushirikiana na wadau wa Afya kwa kuiona changamoto hii iliyokuwa ikitukabili kisha kuamua kuitatua’’ amesema.
Mkuu wa Shirika lisilo la kiserikali la Catholic Relief Services Tanzania (CRS) Taylor Lanton amesema Shirika hilo limetoa Baiskeli 250 ambapo kati ya hizo 200 ni kwa ajili ya wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii pamoja na walimu wa Vijiji kwa ajili ya vikundi vya kuweka na kukopa vijijini ili kuwaaezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Amesema mojawapo ya majukumu ya msingi ya Shirika hilo ni kutekeleza mradi unaolenga kuboresha hali za afya na lishe kwa vijana walio katika rika balehe waliopo shuleni na kwenye Jamii sambamba na wanawake vijana wenye umri kati ya miaka 10 hadi 24 mkoani Kigoma.
‘’Tunaendelea kuangalia zaidi katika kuiongezea nguvu serikali katika kuboresha Afya ya Jamii, uwepo wa lishe bora sambamba na kuboresha maisha ya mtu mmoja mmoja kupitia maeneo hayo, aidha nimefurahishwa na namna mnavyoutekeleza mradi pamoja na ushirikianomkubwa mnaotupa kama uongozi wa mkoa wa Kigoma nasi tunaendelea kuahidi kufanya kazi nanyi’’ amesema Bi. Lyton.
Akizungumza kabla ya kukabidhi vitendea kazi hivyo Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye amesema Serikali ya awamu ya Sita kupitia wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na wadau wa Maendeleo kupitia sekta hiyo ili kukabialiana na changamoto zinazowakabili wananchi hususani katika upatikanaji wa huduma bora za Afya.
Amewataka wanufaika wa vitendea kazi hivyo kwenda kuvitumia kuendana na miongozo waliyopewa ili viweze kuleta ufanisi katika Mapinduzi ya Sekta hiyo muhimu sambamba na kupunguza idadi ya vifo vya wanawake wajawazito na watoto katika maeneo ya vijijini.
‘’Nichukue nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza wahudumu wote wa Afya ngazi ya Jamii mkoa wa Kigoma kwa kazi nzuri mnazozifanya ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha Afya, lishe na Ustawi wa watu wa Kigoma kwa jumla’’amesisitiza Andengenye.
Jumla ya baiskeli 72 zimegawiwa katika halmashauri ya Kigoma, 84 Wilaya ya Uvinza na nyingine 94 zikitolewa kwa wanufaika katika halmashauri ya wilaya ya Kibondo.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa