Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye ameipongeza Serikali kupitia Sekta ya Sheria Nchini kwa kuimarisha matumizi ya Mfumo wa TEHAMA katika kutoa Huduma za kimahakama, hali inayoongeza kasi na kurahisisha mchakato wa kutoa haki kwa wananchi.
Andengenye ametoa kauli hiyo alipozungumza kwenye maadhimisho ya wiki na Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Mwana Centre, Manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo amewataka wananchi kutumia fursa ya uwepo wa maadhimisho hayo kupata Elimu na misaada ya kisheria.
Amesema kuimarika kwa mifumo ya utoaji wa huduma za kisheria kumeendelea kuchangia kuimarisha uchumi wa mkoa Mkoa kwani Maendeleo hutegemea mahitaji makubwa ya kiwango cha haki jambo linaloendelea kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Katika hatua nyingine Andengenye amewataka watumishi wa Mahakama mkoani Kigoma kuendelea kutoa Huduma bora za kisheria kwa kuzingatia wakati ili kuruhusu wananchi kupata muda wa kushughulikia masuala ya kimaendeleo.
‘’Mahakama pekee haiwezi kutoa haki kama wadau wake hawajajipanga na kuboresha mnyororo wote wa utoaji wa Huduma za kisheria’’ amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma Mhe. Augustine Rwizile amesema Serikali inaendelea kuboresha mfumo wa Mahakama mtandao ili kurahisisha na kuimarisha utoaji wa Huduma za kimahaka.
‘’Mahakama imeendelea kutumia mifumo ya kiteknolojia kushughulikia mashitaka mbalimbali kwani kuanzia Novemba 2023, tumekuwa tukitumia mfumo mpya wa Usimamizi wa Kesi, ambapo unawezesha kusajili mashitaka, kupangiwa tarehe na hatimaye kusikilizwa’’amesema Jaji Rwizile.
Maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria yameanza Januari 24, 2024 na yanatarajiwa kuhitimishwa kwa kufikia kilele chake Februari 1, 2024, yakibeba Kauli Mbiu isemayao ‘’umuhimu wa dhana ya Haki kwa ustawi wa Taifa, nafasi ya wadau na Mahakama katika kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai’’
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255738192977
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa