Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye amejiandikisha katika Daftari la mkazi la wapigakura katika Mtaa wa Shede, Kata ya Kigoma katika kituo cha Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Kigoma na kutoa wito kwa wakazi mkoani hapa kujitokeza na kujiandikisha ili waweze kushiriki kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ifikapo Novemba 27, 2024.
Akizungumza mara baada ya kushiriki zoezi hilo, Mhe. Andengenye amesema ni muhimu kwa wakazi kujiandikisha na kuchagua viongozi wanaowataka ambao pia watasaidia kusimamia utekelezaji wa Shughuli za Maendeleo zinazotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita mkoani Kigoma chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesisitiza kuwa, Uchaguzi wa Viongozi katika ngazi ya Kijiji na Mtaa ndicho chanzo na msingi wa Demokrasia nchini , hivyo kutojiandikisha ili kushiriki kupiga kura ni kujinyima haki hiyo muhimu ya kupata kiongozi ambaye atatokana na maamuzi ya wananchi wenyewe.
Aidha Andengenye ametoa wito kwa wakazi mkoani hapa kuendelea kujitokeza kujiandikisha na kuchagua kiongozi atakayeendana na matakwa yao ili kuepuka malalamiko ya kuongozwa na kiongozi ambaye hajatokana na maamuzi yao.
Upande wake Zainab Omary Mkazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji amesema ameshiriki zoezi hilo ili kupata kiongozi ambaye atatokana na maamuzi yake sambaba na kupata haki yake ya kidemkrasia kuendana na Sheria na taratibu za nchi.
Naye Zakaria Philimoni ambaye ni Msimamizi msaidizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kituo cha Meti, Manispaa ya Kigoma Ujiji amesema zoezi hilo linaendelea vizuri huku akitoa wito kwa wakazi kuendelea kujitokeza kwani zoezi halina usumbufu wowote kutokana na serikali kuandaa idadi ya vituo vya kutosha kwa ajili ya wananchi kujiandikisha.
Zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la wakazi linaendelea mkoani hapa huku likitarajiwa kufikia tamati ifikapo Oktoba20,2024.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa