Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amewasisitiza watendaji wa Serikali mkoani Kigoma kusimamia utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa umakini na uadilifu ili kutokuwa kikwazo kwa Serikali katika kupeleka Maendeleo kwa wananchi.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa maelekezo hayo akiwa katika ziara ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa Miradi ya BOOST na SEQUIP katika Halmashauri ya Mji Kasulu, huku akisisitiza suala la ufuatiliaji na kufanya tathimini `wakati wote wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Amesema watendaji wanapaswa kuepuka kuzipa nafasi changamoto na kuwa sababu au vigezo vya kushindwa kufikia malengo yaliyowekwa na serikali, bali watoe taarifa kwa ngazi nyingine za kiserikali ili kupata utatuzi wa vikwazo vinavyojitokeza wakati wa utekelezaji.
‘’Tumepewa nafasi hizi za usimamizi serikalini ili kubaini na kutatua changamoto zinazoleta ukinzani katika kufanikisha hatua mbalimbali zitakazowezesha maendeleo kuwafikia wananchi, hivyo tusiogope kukabiliana nazo na huo ndio wajibu wetu mkubwa’’ amesema Andengenye.
Ameendelea kusisitiza kuwa, watendaji hawana sababu ya kushindwa kukamilisha miradi ya maendeleo wakati serikali inapeleka fedha za kutosha katika maeneo inakotekelezwa miradi hiyo.
Kupitia ziara hiyo Mkuu wa Mkoa ametembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya Ujenzi wa miundombinu mbalimbali kwa ajili ya uboreshaji wa Mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji chini ya program za BOOST na SEQUIP katika Shule ya Sekondari Nyumbigwa Mpya, Muka, Msambara pamoja na Shule za Msingi Kasulu, Nyasha na Kibagwe.
Aidha kukamilika kwa miradi hiyo kunatarajia kupunguza mrundikano wa wanafunzi madarasani, vyooni pamoja na kupunguza umbali kwa wanafunzi kuyafikia maeneo hayo ya huduma za kitaaluma.
Pia baadhi ya wakazi wanaoishi katika maeneo inakotekelezwa miradi hiyo wametanabaisha kunufaika kwao kutokana na miradi hiyo kuchangia upatikanaji wa ajira za muda zinazowasaidia kupata fedha kwa ajili ya kujikimu kimaisha.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa