PICHA: Kikao cha Tathimini ya utekelezaji wa shughuli za uboreshaji na usimamizi wa Elimu Mkoa wa Kigoma Kilichofanyika Januari 20, 2023 katika Ukumbi wa NSSF mANISPAA YA Kigoma-Ujiji.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mhe. Thobia Andengenye amewataka wazazi na wadau wa Elimu kuhakikisha Huduma ya Chakula inaanza kutolewa kwa Shule zote za Msingi na Sekondari katika Mkoa wa Kigoma ili kuimarisha utulivu na usikivu wakati wa utekelezaji wa zoezi la ujifunzaji na ufundishaji.
Melekezo hayo ameyatoa Leo Januari 20, 2023 alipomwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Angellah Kairuki kwenye Kikao Kazi cha Tathimini ya Utekelezaji wa Shughuli za Uboreshaji na Usimamizi wa Elimu Mkoa wa Kigoma kilichowakutanisha Viongozi na Watendaji wa Sekta ya hiyo mkoani Kigoma.
‘‘Kila Mzazi anajukumu la kutoa chakula cha kila Siku katika Familia hivyo sioni sababu ya wazazi kushindwa kutekeleza jukumu hilo muhimu kwa manufaa ya watoto wao ili waweze kupata Afya bora. Pia ikumbukwe, ulishaji wa wanafunzi shuleni utatupunguzia changamoto ya utapiamlo na udumavu Mkoani kwetu na Taifa kwa ujumla’’ amesema Andengenye.
Kwa Mujibu wa Taarifa ya Mapitio ya Tathimini ya utekelezaji wa Shughuli za Uboreshaji na usimamizi wa Elimu Kimkoa, hadi kufikia Januari 19,2023 Idadi ya Shule za Msingi zinazotoa Huduma ya Chakula shuleni kimkoa ni shule 43 kati ya 218 na upande wa Sekondari ikiwa 156 kati ya 708.
Akitoa Taarifa ya Mapitio ya Tathimini ya Utekelezaji wa Mikakati ya Kuboresha Elimu Msingi na Sekondari kwa Mwaka 2022 kwa niaba ya Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, Katibu Mtendaji Tume ya Utumishi wa Walimu Taifa Bi. Paulina Nkwama amesema lengo la kikao kazi hicho ni kujenga uelewa wa pamoja kuhusu namna ya kutekeleza mikakati na utatuzi wa Changamoto zilizobainishwa katika miongozo ya elimu pamoja na kutoa hamasa kwa viongozi, wasimamizi na walimu katika kutekeleza Majukumu yao.
Amefafanua kuwa, Ofisi ya Rais TAMISEMI iliweka vigezo vya Upimaji wa Utendaji kazi kwa ngazi mbalimbali za Uongozi na watendaji katika Tasnia ya Elimu ili kuhakikisha Changamoto za kiutendaji zilizobainika katika Mwaka 2022 zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
‘’Nasisitiza kila mshriki wa kikao kazi hiki atoke na uelewa wa kutosha kuhusu majukumu yaliyoko mbele yake na namna atakavyojipanga ili kufikia malengo yaliyobainishwa katika Miongozo ya Uboreshaji na Usimamizi wa Elimu katika Ngazi zote’’ amesisitiza Nkwama.
Upande wake Afisa Elimu Mkoa wa Kigoma. Paulina Ndigeza amesema hali ya uandikishaji kwa Wanafunzi waliofaulu Drasa la Saba na kutakiwa kuanza Kidato cha Kwanza kwa Muhula wa Masomo 2023 imefikia Asilimia 58.4
‘‘Hadi kufikia Tarehe 19, Januari 2023 Mkoa wa Kigoma kupitia Idara ya Elimu tumefanikiwa kuandiskisha Wanafunzi 12,781 wanaotakiwa kuanza Kidato cha Kwanza ambapo wavulana na 13,019 na Wasichana 12,762 ambapo ni sawa na Asilimia 58.4 ya Wanafunzi wote waliotakiwa kujiunga na Elimu ya Sekondari kwa Mkoa wetu’’ amesema Ndigeza.
Aidha kupitia kikao hicho Muhimu cha wadau wa Elimu mkoani Kigoma wajumbe wameazimia kuwa, wazazi, Uongozi wa Elimu na Serikali pamoja na watendaji wa Idara hiyo, kufuatilia na kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wawe wameandikishwa ifikapo tarehe 31, Januari 2023.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa