Wahitimu wa Mafunzo ya Awali ya kijeshi ya vijana wa kujitolea Oparesheni miaka 60 ya Jeshi la Kujenga kundi la Saba (7) 2023/2024 825 KJ-Mtabila wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya Teknolojia ikiwemo kutumia mitandao ya kijamii kwa malengo ya kujifunza masuala yatakayokuwa na Tija katika maisha yao ikiwemo kujiimarisha kitaaluma na kiuchumi.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye alipozungumza na wahitimu hao, alipokuwa akifunga mafunzo hayo kwenye hafla iliyofanyika katika Kambi ya 825KJ-Mtabila iliyopo wilayani Kasulu mkoani hapa.
Amesema matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yamesababisha baadhi ya watu hususani vijana kujihusisha na mambo yaliyo kinyume na maadili yanayoendana na mila na Desturi za kiafrika.
Andengenye ameupongeza na kuushukuru uongozi wa JKT kwa usimamizi mzuri wa vijana hao mpaka kufikia kuhitimu mafunzo hayo wakiwa wenye sifa na weledi katika kutekeleza jukumu la ujenzi na ulinzi wa Taifa.
''Niwasihi nendeni mkautumie ujuzi mlioupata katika kuzilinda Afya zenu, kujihusisha na shughuli za liuchumi kupitia ujasiriamali ili kuhakikisha mnachangia pato la Taifa sambamba na kutekeleza jukumu la utunzaji wa Mazinngira'' amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Aidha mkuu huyo wa mkoa amewataka wahitimu hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kutumia ujuzi walioupata kujiajiri wakati wakisubiri fursa za ajira huku akiwakumbusha kuwa nchi ina fursa mbalimbali za kujitafutia kipato iwapo watajiamini na kutumia maarifa waliyonayo.
Akimwakilisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Hawa Kodi ambaye ni Mkuu wa Tawi la Ugavi na Uhandisi JWTZ ametoa wito kwa wahitimu hao kuyaishi maisha yatakayosadifu mafunzo waliyoyapata.
Aidha Jenerali Kodi amewataka wahitimu hao wakawe chachu katika kuhamasisha vijana wengine wenye sifa kujiunga na JKT ili waweze kupata Stadi mbalimbali za maisha zitakazowawezesha kujiajiri na kujipatia kipato.
Upande wake Brig. Jen. Hassan Mabena amesema kiapo cha Utii walichoapa vijana hao ni ishara tosha ya Taifa kuendelea kuwa salama kutokana na kuwa na vijana wengi wenye mafunzo na utayari katika kulinda Amani ya nchi.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo katika ujasiriamali na kuwapa maarifa na stadi za maisha zitakazowafanya waweze kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa