Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema Serikali mkoani hapa itaendelea kuweka Mazingira bora na rafiki kwa ajili ya kuzidi kuvutia wawekezaji kwa lengo la kuzalisha fursa za ajira na kuinua uchumi wa wakazi na Taifa kwa ujumla.
Andengenye ametoa kauli hiyo alipotembelea na kukagua eneo Maalum la uwekezaji mkoani Kigoma (KiSEZ) na kuwataka waliopata fursa za ajira kupitia uwekezaji unaofanyika katika eneo hilo kufanya kazi kwa bidi na uaminifu ili kuwafanya wawekezaji kupata matokeo chanya kupitia uwekezaji wanalioufanya na kutoa fursa kwa wafanyakazi kupata ajira kwa muda mrefu.
Amesema iwapo watendaji hao watakuwa waaminifu na kuzalisha kwa ubora na kiwango kilichowekwa, hali hiyo itawavutia wawekezaji wengine sambamba na wale waliopo kutanua shughuli zao kutokana na kupata matokeo chanya kupitia uwekezaji wanaoufanya.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amewaalika wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kutumia fursa ya kuwekeza katika eneo hilo ambalo serikali ya mkoa imekwisha liwekea miundombinu ya Umeme, Maji na Barabara ili kulifanya kufikika na kurahisisha michakato ya uchukuzi.
Amesisitiza kuwa, suala la uwekezaji hususani kwenye viwanda vya kuzalisha vifaa vya ujenzi litapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za manunuzi ya vifaa hvyo kwa wakazi wa mkoa wa Kigoma pamoja na mikoa na nchi jirani
Eneo la uwekezaji la KiSEZ lina ukubwa wa Hekta 691 likiwa na viwanja vilivyopimwa zaidi ya 400, ambapo linamilikiwa kwa pamoja na Manispaa ya Kigoma Ujiji pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ambapo mpaka kufikia Novemba 2024 jumla ya wawekezaji 10 tayarai wanaendesha shughuli zao ikiwemo uzalishaji pamoja na ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa