Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mhe. Thobias Andengenye amewataka watendaji wa Serikali kusimamia miradi inayotekelezwa na Serikali kwa ukaribu na umakini mkubwa ili iweze kukamilika kwa wakati na kiwango sahihi kuendana na miongozo ya Serikali.
Mkuu wa Mkoa ametoa Melekezo hayo alipofungua kikao kazi cha Tathmini ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa Mwaka 2022/2023 kwa Mkoa wa Kigoma, kilichowakutanisha Wakuu wa wilaya, Makatibu Tawala wilaya, Wakurugenzi, pamoja na wakuu wa Idara na Vitengo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
‘‘Ipo changamoto kwa baadhi ya watendaji wenye dhamana kutosimamia kwa ukaribu Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa na serikali na kusababisha baadhi ya kazi kutofanyika kwa kuzingatia Miongozo na Maelekezo yanayotolewa na Serikali, hali inayoweza kusababisha baadhi ya miradi kutekelezwa chini ya kiwango au kinyume na miongozo ya Serikali’’ amesema Andengenye.
Ameendelea kusisitiza kuwa, watendaji waache kuorodhesha changamoto na kuzitumia kama kisingizio cha kutotekeleza Miradi kwa ufasaha na kwa wakati uliopangwa, bali wajikite katika usimamizi wa karibu na kuikagua miradi hiyo mara kwa mara huku wakizingatia miongozo inayotolewa na Serikali katika utekelezaji wa kazi hizo.
Naye Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Albert Msovela amewataka wakuu wa vitengo vya Manunuzi katika Halmashauri kuongeza ufanisi na kuzingatia muda katika kufanya manunuzi ya vifaa vya ujenzi ili kuharakisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo mkoani Kigoma.
Amesisitiza kuwa, vitengo vya Manunuzi katika maeneo mengi vimekuwa changamoto katika kuhakikisha manunuzi yanafanyika katika muda uliopangwa hali inayosababisha miradi mingi inayotekelezwa kutokukamilika kwa wakati.
Pia amewaasa watendaji wa Serikali kuongeza ushirikiano na kudumisha mahusiano mema katika utendaji kazi ndani ya Mkoa jambo litakalorahisisha uwepo wa mawasiliano ya karibu na kufikiwa kwa malengo ya kiutendaji.
Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Ester Mahawe amewashauri wakurugenzi na wakuu wa Idara na vitengo vinavyosimamia utekelezaji wa kazi za Maendeleo kutembelea mara kwa mara maeneo ya utekelezaji ili waweze kubaini dosari zinazojitokeza na kuzifanyia kazi kwa wakati kabla ya kukamilika kwa miradi hiyo.
‘‘Namna bora ya kudhibiti changamoto katika miradi yetu tunayoitekeleza ni kuhakikisha miongozo na Maelekezo yanayotolewa na Serikali yanazingatiwa. Baadhi ya watendaji katika maeneo ya utekelezaji wamekuwa wakifanya kazi kinyume na taratibu, ili kudhibiti mapungufu yanayoweza kujitokeza suluhisho ni kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kutoa maelekezo kuendana na miongozo ya Serikali’’ amesema Mahawe.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa