KATIBU TAWAL A MKOA WA KIGOMA HASSAN RUGWA AKIZUNGUMZA WAKATI AKIZINDUA MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA FAMILIA KIMKOA LEO MEI 9,2024 AMBAYO KILELE CHAKE ITAKUWA MEI 15/2024/
Wakazi mkoani Kigoma wametakiwa kuendelea kuimarisha ustawi wa familia na Jamii kwa ujumla ili kuepuka changamoto za kimalezi zinazotokana na migogoro ya kifamilia na kuathiri makuzi ya watoto.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa alipozungumza kwenye uzinduzi wa Siku ya kimataifa ya Familia duniani kimkoa, ambayo Maadhimisho yake hufanyika kila ifikapo Mei 15 na kuwataka wazazi mkoani hapa kutoyumbishwa na uwepo wa changamoto za kiuchumi katika kusimamia suala la malezi bora ya watoto wao.
Amesema kukosekana kwa malezi bora ya wazazi kumeendelea kusababisha watoto wengi kujisimamia kimalezi na kujifunza tabia na desturi mbalimbali kutokana na makundi wanayoishi nayo, jambo ambalo ni hatari kwa jamii au familia husika kutokana na watoto hao kuwa na mienendo tofauti na ile ya wazazi wao.
Ameendelea kusema jukumu kubwa la malezi katika jamii limeachwa kwa wanawake pekee huku wazazi wa kiume wakijielekeza zaidi katika shughuli za utafutaji wa maisha na hata baadhi kutelekeza kabisa familia zao, jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa kuendelea kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili.
‘’Wazazi wenye nafasi kubwa kiuchumi ndio wamethibitika kuwa na changamoto kubwa za kimalezi kutokana na kukasimisha jukumu la malezi kwa watumishi wa ndani pamoja na walimu wa shule hali inayochangia watoto wengi kujifunza tabia zisizo za asili ya familia wanazotoka’’ amesema Rugwa.
Katika hatua nyingine Rugwa amesema maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano sambamba na kutuletea mapinduzi makubwa ya kimawasiliano, yamekuja na mila na desturi za kigeni ambazo zimeendelea kuathiri utamaduni na mwenendo wa asili wa jamii za kiafrika.
Ameyataja matokeo ya changamoto za kimaadili katika Jamii kuwa ni pamoja na utovu wa nidhamu, kukosa ushirikiano na mahusiano mema miongoni mwa wanajamii, wazazi kushindwa kushirikiana katika matunzo ya watoto ikiwemo ukosefu wa lishe bora pamja na usimamizi wa watoto kitaaluma hali inayosababisha uwepo wa ongezeko la vitendo vya ukatili wa kingono, kisaikolojia na kihisia.
Aidha amelitaja suala la baadhi ya wazazi kushindwa kutoa mahitaji ya msingi kwa watoto wao, kukosa muunganiko baina ya wazazi, kukosekana kwa upendo miongoni wa wanajamii kuendelea huchangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa malezi yasiyo na maadili.
Naye Mchungaji Justin Sologo kutoka umoja wa makanisa ya kikristo Tanzania, Mkoa wa Kigoma amesema changamoto kubwa inayoikabili jamii ya sasa ni watoto kuiga mila na desturi zilizo nje ya tamaduni zetu pamoja na miongozo ya kidini.
‘’Kanisa linajukumu kubwa la kurudisha mahusiano mema na mienendo itakayokuwa salama kwa jamii yote hususani kwa watoto kutokana na kutumia muda mwingi wa maisha yao kujumuika na makundi mbalimbali’’ Amesisitiza Sologo.
Dkt Haroun Shaaraw ambaye ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Ustawi wa Jamii ya Kiislamu mkoani Kigoma amesema wazazi wanaposhindwa kutekeleza jukumu la kuadilisha vijana wao kwa kuzingatia misingi ya dini jamii itajikuta inaendelea kuwa na kizazi kisicho na maadili na kutokuwa na hofu ya Mungu.
‘’Kwa sasa asilimia kubwa wazazi wanashindwa kusimamia maadili ya watoto kutokana na wazazi wenyewe kutokuwa na uelewa na maadili ya kutosha na kushindwa kuhamisha maarifa hayo kwa watoto wao. Msingi bora wa malezi ya watoto huanza kutengenezwa kutoka ngazi ya familia kisha kwenda katika jamii ili waweze kuiga mambo mema kwa ajili ya kuwasaidia kuishi maisha yanayokubalika katika jamii’’ amesema Dkt. Haroun.
Amefafanua kuwa rasilimali watu lazima ijengwe katika msingi wa kumhofia Mungu kuanzia nyumbani, katika nyumba za ibada, shuleni na katika jamii inayomzunguka, hapo Taifa litakuwa na uhakika wa kuwa na kizazi chenye maadili na kufuata mila na desturi zenye tija kwa taifa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa