Wakazi wilayani Buhigwe Mkoani hapa wameiomba Serikali kuendelea kusimamia ahadi inazozitoa katika utekelezaji wa miradi ya Maendeleo ili iweze kukamilika kwa wakati na kuondoa adha kwa wananchi.
Kauli hiyo imekuja kufuatia agizo la Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa kumtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe kuhakikisha Kituo cha Afya Kajana kilichoanza ujenzi wake Mwaka 2021 kinafunguliwa na kuanza kutoa Huduma ifikapo Mei 28, 2024.
Amesema serikali haitomvumilia mtumishi yeyote wa Umma atakayebainika kukwamisha utekelezaji wa Maagizo maelekezo ya usimamizi wa Miradi kwani hali hiyo inasababisha migogoro baina ya wananchi na serikali yao sambamba na kuchelewesha maendeleo.
Amesema wenye jukumu la usimamamizi wa miradi hiyo wanapaswa kujitathmini huku akisisitiza kuwa iwapo kuna mtendaji wa serikali anabainika atasababisha mkwamo katika utekelezaji wa miradi ya kutolea huduma kwa wananchi, Serikali haitosita kumchukulia hatua.
Sambamba na hilo, Katibu Tawala huyo amesema agizo hilo linapaswa kwenda sambamba na ukamilishwaji wa miundombinu ya Nyumba za watumishi, tanki la Maji pamoja na choo katika Zahanati ya Kijiji Kasumo, ili kuruhusu wananchi kupata huduma za kiafya katika maeneo ya jirani na makazi yao.
Upande wake Mganga mkuu wa Mkoa wa Kigoma Jesca Lebba amesema Ofisi yake imepokea maelekezo hayo hivyo itashirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ili kuhakikisha huduma za Afya zinaanza kutolewa katika maeneo yaliyoelekezwa ifikapo Mei 28,2024.
‘’Tunaahidi kuhakikisha tunaleta hapa wataalam wa Afya pamoja na vifaa vya kuanzia hususani katika jengo la wagonjwa wa nje ili ifikapo Mei 28,2024 huduma za msingi za awali zianze kutolewa wakati tunaendelea kukamilisha uwekaji wa vifaa kwa ajili ya utoaji wa huduma kubwa kama zile za upasuaji’’ amesema Lebba.
Akitoa ufafanuzi kuhusu changamoto zinazosababisha kuchelewa kwa ujenzi huo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ugavi na Manunuzi katika Halmashauri hiyo Godwin Nsemwa amesema kumekuwa na changamoto ya manunuzi ya vifaa kutokana na kuhcelewa kwa michakato ya kuwapata wazabuni kwa ajili ya kuiuzia Halmashauri zana za ujenzi.
Upande wao baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wamesema watendaji wa Halmashauri hiyo wameshindwa kuishirkisha kwa ufasaha kamati ya manunuzi na badala yake wamekuwa wakijichukulia maamuzi bila kuishirikisha kamati hiyo hali inayowafanya kushindwa kufahamu msingi wa kutofikiwa kwa malengo ya ujenzi.
‘’Ujenzi wa Kituo hiki cha Afya ulianza kwa hatua za awali mwaka 2021 mara baada ya Halmashauri kupokea kiasi cha shilingi mil.500 lakini mpaka sasa kazi mbalimbali zimeendelea kusuasua hali inayotupa changamoto ya kupata huduma bora za kiafya kutokana na huduma hizo kupatikana maeneo ya mbali’’alisema Januari Luckas Mkazi wa Kajana wilayani humo.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa